Wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wamehimizwa kufika na kujipatia huduma ya sheria bila malipo katika Kliniki ya Sheria inayofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano na Kamati ya Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi ya Moshi.
Akizungumza wakati Kliniki hiyo Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Dickson Mbilu ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza zaidi kupata huduma za ushauri wa kisheria zinazotolewa bure na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku akiridhishwa na mwitikio wa wananchi wanaokuja katika kliniki hiyo.
“Mwitikio ni mzuri wananchi wanakuja kwa wingi kupata msaada wa kisheria, pia nitumie nafasi hii kuwakumbusha kuwa kilele cha kliniki yetu ni tarehe 27 Januari hivyo waendelee kuja sisi tuko tayari kuwahudumia”. Alisema Wakili Mbilu.
Kwa upande, wake Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Kamati ya Sheria ya mkoa wa Kilimnajaro Bi. Glorian Issangya ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanya Kliniki ya Sheria bila malipo katika mkoa wa Kilimanjaro, kwakuwa imesaidia kutatua matatizo ya wananchi wengi waliokuja kupata huduma katika kliniki hiyo.
“Niipongeze sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanya jambo hili, kliniki hii imekuwa na faida kwa wananchi wetu kwani kliniki hii imeweza kutatua kero mbalimbali za kisheria zilizokuwa zinawakabili.” Amesema Bi. Glorian Issangya
Aidha Bi. Glorian Issangya ameeleza kuwa Kamati ya mkoa wa Ushauri wa Kisheria imejipanga kutembelea kwenye maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wa Kilimanjaro kutatua changamoto za kisheria kwa wananchi wa mkoa huo.
“Kamati ya Mkoa ya huduma za kisheria inajipanga kuwatembelea wananchi katika maeneo yao hususani vijijini ili tuweze kutatua migogoro yao na kuwafanya wananchi wetu wajikite kwenye shughuli za maendeleo.” Alisema Wakili Glorian Issangya
Nae, Bw. David Mongi amesema kuwa kliniki hiyo imekuwa msaada na mkombozi kwa wananchi wengi, kwa kutatua migogoro mbalimbali ndani ya muda mfupi na pia imewasaidia watu ambao wenye kipato cha chini kwakua kliniki hiyo imekuwa ikitoa ushauri na msaada wa kisheria bila malipo.
“Mimi nimehudhuria Kliniki hii kwakweli nimefarijika sana na huduma hii, naishuruku Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta jambo hili, nimehangaika muda mrefu na jambo langu lakini jopo hili la Mawakili limenihudumia naona likimalika kwa haraka”. Amesema Bw. Mongi
Kliniki ya Sheria kwa Wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro ilianza tarehe 21 Januari 2025 katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi ya Moshi, itafikia kilele chake kwa mkoa wa Kilimanjaro tarehe 27 Januari, 2025.