Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mara umetangaza rasmi kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya uteuzi wake kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katika mkutano huo maalum wa CCM, pia walimteua Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza, huku Dkt. Hussein Mwinyi akiteuliwa kugombea nafasi ya urais kwa upande wa Zanzibar.
Akizungumza leo Jumapili, Januari 26, 2025, mjini Musoma, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara, Mary Daniel, alisema kuwa wanawapongeza wagombea wote walioteuliwa na wanatoa tamko la kuwaunga mkono kikamilifu.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa jukumu la sasa ni kuhakikisha wanatafuta kura kwa ajili ya ushindi mkubwa wa wagombea hao.
“Kazi ndiyo inaanza. Sisi Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Mara mbali na kuwapongeza wagombea wetu, tunatoa tamko la kuunga mkono uamuzi wa mkutano mkuu maalum wa CCM. Tunalo jukumu moja tu mbele yetu—kutafuta kura ili wagombea wetu washinde kwa kishindo katika uchaguzi ujao,” alisema Mary Daniel.
Aidha, Mary alisema serikali chini ya uongozi wa CCM imeweza kutekeleza ilani yake kwa mafanikio makubwa, akibainisha kuwa Mkoa wa Mara umepokea zaidi ya Sh1.22 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kijamii katika kipindi cha miaka mitatu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, alisema kuwa wana-CCM sasa wana jukumu kubwa la kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushika dola kupitia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi.
“Hatuna cha kumlipa Mama zaidi ya kumpa kura. Ilani ya CCM imetekelezwa vizuri sana, na hapa kwetu tumeshuhudia miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari, ambayo zamani wazazi walilazimika kuchangia fedha, lakini sasa inatekelezwa na serikali,” alisema Chandi.
Katibu wa Kamati ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Mara, Juma Masirori, aliunga mkono tamko la UVCCM huku akieleza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unalenga si tu kuboresha huduma kwa wananchi, bali pia kuimarisha amani ya nchi.
“Mama Samia amefanya mengi mazuri kwa ajili ya nchi yetu. Kitu kikubwa zaidi ni kudumisha amani, ambayo ni msingi wa maendeleo. Penye maendeleo pana amani,” alisema Masirori.
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa amani ya nchi ni muhimu kwa ustawi wa kiuchumi wa taifa na wananchi kwa ujumla.