DAR ES SALAAM
Katika juhudi za kuitumia fursa ya Mkutano wa Afrika wa Nishati unaotarajiwa kuanza kesho, Januari 27, 2025, jijini Dar es Salaam, Wizara ya Maliasili na Utalii imejidhatiti kuimarisha taswira ya Tanzania kama kivutio cha kipekee cha utalii.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, akizungumza leo Januari 26, 2025, alibainisha kuwa maandalizi yamekamilika kwa kuhakikisha vivutio vya utalii vinawasilishwa vyema kwa wageni wa mkutano huo wa kimataifa. Dkt. Abbasi, akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu (Utalii) Nkoba Mabula, Mkurugenzi Mkuu wa TTB Ephraim Mafuru, na viongozi wengine waandamizi, alitembelea maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuvutia wageni, yakiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1, 2, na 3), pamoja na maeneo ya Ocean Road na Aga Khan.
“Kila eneo tumelipamba kwa taswira halisi za utalii wetu, zikiwemo ngozi za wanyama na picha za mandhari ya kuvutia, ili kuwapa wageni taswira ya kile ambacho nchi yetu inatoa katika sekta ya utalii,” alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, alibainisha kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tayari imeandaa safari za wageni kwenda maeneo ya vivutio vya utalii. “Kuna maafisa waandamizi wa Benki ya Dunia wanaotarajia kutembelea Serengeti, na tunaendelea kuratibu ziara za wageni wengine wengi. Tanzania iko tayari kuwakaribisha wote,” aliongeza.
Mkutano wa Africa Energy Summit umevutia viongozi waandamizi, wawekezaji, na washiriki kutoka mataifa mbalimbali, na ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kujitangaza kimataifa siyo tu kama kitovu cha nishati, bali pia kama mahali pa kipekee kwa utalii wa kipeo cha juu.