Dotto
Mwabale na Solomoni Philemon, Singida
SERIKALI
kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imetoa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. Milioni 210 katika Hospitali ya Wilaya ya Itigi iliyopo Mkoa wa Singida.
Meneja wa MSD Kanda ya Kati, Mwanashehe Jumaa akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Januari 24, 2025 alisema mwishoni mwa mwaka jana walipokea maombi ya mahitaji ya vifaa hivyo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Itigi yenye thamani ya Sh. Milioni 300.
Alisema baada ya kupokea maombi hayo walianza kufanya mchakato wa kuvipata ambapo jana walipeleka vifaa vyenye thamani ya Sh. Milioni 210 na kuwa vifaa vilivyosalia watahakikisha vinapelekwa siku chache zijazo ili malengo tarajiwa ya
kuhakikisha vifaa hivyo vinaanza kutumika kwa kutoa huduma za afya kwa
wananchi.
“ Tunaimani kwa matumizi ya vifaa hivi tutafanikiwa kukabiliana na uzazi pingamizi na changamoto zingine zinazohusu uzazi,”
alisema Jumaa.
Jumaa alitaja baadhi ya vifaa walivyovikabidhi kuwa ni mashine ya usingizi, vitanda vya kujifungulia, meza, vitanda kwa ajili ya kufanyia upasuaji, taa za kufanyia upasuaji, mashine inayotumika kufanyia usafi vifaa vinavyotumika kufanyia
upasuaji, mashine ya kufulia na mashine inayotumika kupimia urefu na uzito
watoto.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha nyingi za kununulia vifaa hivyo kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Itigi,” alisema Jumaa.
Aidha Jumaa aliomba vifaa hivyo vifungwe haraka ili viweze kuanza kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itigi, Emanuel Mallange alisema kukabidhiwa kwa vifaa hivyo ni hatua nzuri ya kuanza rasmi kutoa huduma katika hospitali hiyo.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alitupatia Sh. Milioni 300 ambazo tulizipeleka MSD kupitia ofisi ya Mkurugenzi ambao leo hii wametuletea na kuvipokea vifaa hivi,” alisema Mallange.
Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Vicent Mashinji, akipokea vifaa hivyo alihimiza hadi Machi 1,
2025 vifaa hivyo view vimefungwa na kuanza kufanya kazi.
Mashinji alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea maendeleo makubwa wananchi huku akimnukuu Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere ambaye alisema ukiwa na maendeleo ya vitu bila ya kuwa na maendeleo ya watu ni kazi bure na kueleza kuwa Rais Samia amefanikiwa kwa hilo kwani anafanya vyote viwili kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Ayoub Kambi
aliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vinakwenda kutoa huduma za afya kwa wanananchi hasa kwa wanawake na watoto.