Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ameelezea umuhimu wa kuharakishwa kwa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Kata ya Makanya, Tarafa ya Chome/Suji, ambacho kitakuwa mkombozi kwa vijana wengi wasio na ajira pamoja na ambao wamejikuta wakiingia kwenye kilimo na matumizi ya madawa ya kulevya aina ya mirungi ambayo serikali inapiga sana vita.
Mhe. Kasilda amesema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Tarafa ya Chome/Suji ambapo alisisitiza kuwa kukamilika kwa chuo hicho kutatoa fursa kwa vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa, hivyo kuinua uchumi wao na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla.
“Chuo hiki cha VETA ni mkombozi mkubwa kwa vijana wetu wa wilaya ya Same, Serikali ya Rais Samia inawapenda sana vijana ndio maana imeamua kuleta fedha ili kutekeleza mradi huu wenye lengo la kuwasaidia vijana waweze kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa kwa urahisi” alisema Mhe Kasilda.
Akizungumza kuhusu changamoto zilizochelewesha mradi huo, alieleza kuwa serikali ya wilaya itaziwasilisha kwenye mamlaka za juu ikiwemo wizara husika ili kuhakikisha zinatatuliwa haraka na ujenzi unakamilika. Aidha, alitoa wito kwa wahusika kutunza nyaraka na vifaa vya ujenzi ili kuhakikisha mradi huo unasimamiwa kwa ufanisi.
“Tayari Serikali ya Wilaya tumebaini changamoto ambayo imepelekea ucheleweshaji wa huu mradi hivyo tutawasilisha changamoto tulizozibaini kwenye wizara husika ili itusaidie kukamisha huu mradi huo ambapo mpaka sasa fedha zaidi ya milioni 300 zimetolewa na zimeshatumika kati ya bilioni1.4 zilizotakiwa kutolewa kwa awamu ya kwanza”. Alisema Mhe Kasilda.
Pia amehimiza thamani ya fedha kuendana na ubora wa mradi, akisisitiza kuwa matumizi mazuri ya rasilimali ni muhimu katika kuhakikisha chuo hicho kinakuwa na miundombinu bora kwa ajili ya wanafunzi.
Wananchi wa Makanya wamepokea kwa furaha hatua hiyo, wakieleza matumaini yao kuwa chuo hicho kitakuwa suluhisho la changamoto za ajira kwa vijana na kusaidia kutokomeza kabisa kilimo na matumizi ya dawa za kulevya aina ya mirungi ambayo wamekuwa wakijihusisha nayo kutokana na kukosa shughuli mbadala za kufanya licha ya serikali kupiga vita matumizi ya madawa hayo.