*Kituo mama cha CNG katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhudumia magari 1,200 kwa siku
*Serikali yaendelea kuhamasisha Sekta binafsi ujenzi wa vituo vya CNG
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imepongezwa kwa ujenzi wa mradi wa Kituo mama cha gesi iliyoshindiliwa yaani Compressed Natural Gas (CNG) na Vituo vidogo viwili vya kupokea na kuhifadhi CNG kwa wateja wa awali.
Pongezi hizo zimetolewa Januari 25, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo David wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha kujazia gesi kinachojengwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kujionea maendeleo ya kituo cha kupokea gesi asilia cha Kinyerezi.
“Tunaipongeza Serikali kwa kupokea ushauri wa Bunge kwa kujenga kituo hiki kikubwa cha kujazia gesi kwenye magari ambacho kitasaidia vituo vingine vidogo kuchukua gesi katika kituo hiki ili kwenda kujaza magari katika maeneo mengine,” amesema Mhe.David
Aidha, Kamati ya Bunge imeishauri Serikali kufikiria namna bora ya kusambaza miundombinu ya kusafirisha gesi ili iweze kufika maeneo mengi nchini ili kuendelea kuwapatia fursa wananchi kuendesha mitambo kwa kutumia gesi asilia badala ya mafuta kama ilivyozoeleka.
Mhe. David amesema kusafirisha gesi kwa kutumia mtandao wa bomba ni nafuu zaidi kuliko kutumia magari, na gesi inatakiwa kutumika mikoa yote kwa kuwa itapunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta kama dizeli na Petroli.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema sambamba na kituo hicho kutoa CNG kwa ajili ya kusambaza katika vituo vidogo ambavyo havijaunganishwa na miundombinu ya mabomba ya kusambaza gesi, kutakuwa na huduma ya kujaza CNG kwenye magari ya aina yote ikiwemo malori, mabasi, gari ndogo za abiria na pikipiki za miguu mitatu (bajaji).
“Kituo kitaweza kuhudumia magari manane kwa wakati mmoja na kwa siku kitatoa huduma hii kwa magari 1,200 na hiki ndio kituo chenye uwezo mkubwa kuliko vituo vyote vilivyopo sasa nchini,” amesema Kapinga.
Amesema gharama ya ujenzi wa mradi huo ni shilingi 18, 946, 766, 486 ambazo zimegawanyika katika mikataba mitatu Mother station, Muhimbili station na Kairuki station na fedha yote inagharamiwa na Serikali kupitia TPDC.
Mhe. Kapinga amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari, jambo ambalo limepokelewa vizuri.
Vituo hivyo vinaendelea kujengwa ili kuhakikisha huduma ya kujaza gesi kwenye magari inapatikana katika maeneo mbali mbali nchini kwa kuanza na Mkoa wa Dar es salaam.