Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb), amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, ambapo alikutana na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai, viongozi wa vijiji, na madiwani katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.
Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kujadili matumizi bora ya ardhi miongoni mwa jamii ya wafugaji wa Monduli na kushughulikia changamoto mbalimbali za matumizi ya ardhi zilizojitokeza hivi karibuni. Aidha, Waziri Tax alipata fursa ya kupokea taarifa kuhusu mafunzo ya kijeshi yanayofanyika katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri Tax, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe. Fred Lowassa, alimshukuru kwa kuitikia mwaliko wa haraka na kufika wilayani humo kwa lengo la kujadiliana na viongozi wa kimila wa jamii ya wafugaji na wakulima. Alibainisha kuwa mkutano huo ni hatua muhimu katika kutatua changamoto zinazohusiana na matumizi ya ardhi na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi wa Monduli.
Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Tax aliwahakikishia wananchi wa Monduli kuwa matumizi salama ya ardhi yataendelea kuwepo, hususan katika maeneo yanayomilikiwa na JWTZ. Alisisitiza umuhimu wa kudumisha na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya wananchi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
“Serikali itahakikisha taratibu zote za kisheria zinafuatwa kwa haki na usawa ili kila mmoja apate stahili yake bila ubaguzi,” alisema Waziri Tax.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Shem Kiswaga, viongozi wa jamii ya wafugaji wa Kimasai, uongozi wa halmashauri ya Monduli, pamoja na viongozi waandamizi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Ziara ya Waziri Tax ni ishara ya dhamira ya serikali ya kushughulikia changamoto zinazohusiana na matumizi ya ardhi wilayani Monduli na kuhakikisha masuala hayo yanatatuliwa kwa njia ya maelewano na ushirikiano.