Na. Jacob Kasiri – Mikumi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikari Ndg. Gerson Msigwa akagua na kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege Kikoboga, Mradi unaotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Akiwa katika uwanja huo, Ndg. Gerson Msigwa alishuhudia ndege zaidi ya tano za mashirika tofauti zilizokuwa zimeshusha na kusubiria watalii kutoka mataifa mbalimbali.
Hata hivyo, Msemaji Mkuu huyo alisema, “Serikali imejidhatiti kuboresha viwanja vingi vya ndege katika Hifadhi za Taifa Tanzania ili kuwarahishia watalii wetu kufika hifadhini kwa wakati na kupata ile thamani ya fedha wanazotoa.”
Aidha aliongeza, “Leo tumekiona kiwanja hiki kimoja lakini serikali kupitia mradi wa “REGROW” pia, inaendelea kukamilisha viwanja vingine vya ndege vyenye hadhi na ukubwa wa aina hii katika Hifadhi za Taifa Ruaha na Nyerere. Hivyo kukamilika kwa viwanja hivi na miundombinu mingine ya kisasa katika medani ya utalii itaongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli na kasi ya ukuaji wa sekta hii nyeti kwa faida ya taifa letu.”
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi – Augustino Massesa ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi alisema, “Ndege nyingi tunazozipokea katika hifadhi hii hutokea Zanzibar na zimeendelea kuleta matokeo chanya na tunatarajia siku za usoni tutakuwa na watalii wengi mithili ya wale wanaotembelea Serengeti.”
Akitoa Maelezo ya Kiwanja hicho kwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Afisa Uhifadhi Mwandamizi Herman Baltazari alisema kuwa Uwanja huo ni wa kisasa na umekidhi vigezo vinavyokubalika na Mamlaka ya Viwanja vya ndege kwani una urefu wa kilometa 2.4 kwenye njia ya miruko, kuna jengo la abiria lenye uwezo wa kutosheleza abiria 140 kwa wakati mmoja, majengo ya zimamoto na nishati itakayotumika katika uwanja huo sambamba na eneo la kuegesha magari yatakayokuja kupokea au kuleta wageni wanaoondoka.
Mbali na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya hifadhi hiyo huku shauku kubwa aliyokuwa nayo ni kumuona Kasongo (Ngiri), pia Ndg. Msigwa alikagua mradi wa ujenzi wa “Cottages” pamoja na Uwanja wa mpira wa miguu uliopo ndani ya hifadhi hiyo.
Wakati akiukagua uwanja huo wa mpira wa miguu, Msemaji huyo alisema kuwa Serikali itashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uangalizi wa TANAPA kuhakikisha uwanja huo unaboreshwa ili kukidhi viwango vinavyokubalika na TFF na CAF ili timu kubwa zinazoshiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa waweze kuutumia.
Mkutano huo wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa umefanyika leo Januari 25, 2025 ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, huku waandishi wa Habari wakishuhudia makundi mbalimbali ya watalii huku pembeni wakifurahia kuona wanyamapori.