Na Fauzia Mussa
Wizara ya Maji, Nishati na Madini kupitia Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) imeingia mkataba wa Makubaliano ya Kuuziana Umeme (PPA) wa megawati 200 na Kampuni ya Aseel Oilfield Services yenye makao makuu Dubai, ikishirikiana na Kampuni ya SANY Renewable Energy kutoka Beijing, China. Umeme huo utazalishwa kwa kutumia nguvu ya upepo.
Hafla ya kutiwa saini kwa mkataba huo ilifanyika katika Ukumbi wa ZURA, Maisara, mjini Unguja, na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali. Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi, alisema mradi huo utasaidia kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja cha nishati na kuimarisha upatikanaji wa nishati ya kutosha na endelevu kwa wakazi na viwanda vya Zanzibar.
Kilangi alieleza kuwa mradi huo utafanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itazalisha megawati 120, ikihusisha megawati 100 kwa Unguja na megawati 20 kwa Pemba, ndani ya kipindi cha siku 360.
Mradi huo utawekwa katika kiwanda cha upepo cha Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, eneo linalofaa kutokana na uwezo wake wa kuzalisha upepo wa kutosha pamoja na miundombinu iliyopo.
Katibu Mkuu alisisitiza kuwa mradi huo unaendana na maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anayetoa kipaumbele kwa uwekezaji wa nishati mbadala kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Aseel Oilfield Services, Saeed Al-Jabry, alisema mradi huo ni hatua kubwa kwa Zanzibar na juhudi za kimataifa za nishati endelevu. Alibainisha kuwa mradi huo utasimamia ujenzi na ufungaji wa mitambo ya upepo kwa viwango vya kimataifa, ukigharimu dola milioni 180 za Kimarekani.
Meneja Mkuu wa ZECO, Haji Mohamed Haji, alisifu mchango wa sekta binafsi katika miradi ya nishati Zanzibar na kueleza kuwa mradi huu utahakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika, huku ukichangia kukuza uchumi wa jamii na maendeleo ya viwanda.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza utegemezi wa nishati kutoka nje, kuimarisha usalama wa nishati, na kupunguza gharama.
Hivi karibuni, Rais Dk. Mwinyi alihimiza umuhimu wa miradi ya nishati mbadala katika kufanikisha lengo la Zanzibar kuwa kinara wa nishati safi kikanda, hatua inayotarajiwa kuvutia wawekezaji na kuongeza ajira kwa wananchi wa Zanzibar.