Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhi Tuzo za Mlipakodi Bora wa mwaka 2023/24 Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Januari, 2025.
………………
MAELEKEZO KUHUSU KUTOLIPA KODI YATOLEWE KWA MAANDISHI SI KWA MDOMO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa hajawahi kutoa maelekezo ya kuagiza mtu au shirika lolote kutolipa kodi. Ameeleza kuwa ikiwa kuna sababu ya kutoa maelekezo kama hayo, yatafanyika kwa maandishi rasmi badala ya maagizo ya mdomo.
“Mimi sijawahi kutoa maelekezo mtu asilipe kodi, na ikitokea haja ya kufanya hivyo, nitatoa maelekezo kwa maandishi, sio mtu aje kwa mdomo,” alisema Rais Samia huku akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Januari 23, 2025, wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walipa kodi bora wa mwaka 2023/2024, iliyofanyika katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Rais Samia ameeleza kuwa ulipaji kodi ni msingi wa maendeleo ya taifa, huku akitoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unafanyika kwa ufanisi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, na walipa kodi waliotunukiwa tuzo kwa mchango wao mkubwa katika kuiwezesha nchi kufanikisha malengo ya mapato kwa mwaka uliopita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhi Tuzo za Mlipakodi Bora wa mwaka 2023/24 kwa wafanyabiashara wanaomiliki Makampuni mbalimbali kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Januari, 2025.