DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
WAFANYAKAZI wa Kituo cha Kimataifa cha Mkutano Arusha (AICC), wamejipanga kutoa huduma bora kwa Wakuu wa nchi za Afrika ambao watashiriki Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Nishati, utakaofanyika Januari 27 na 28 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere JNICC jijini Dar es salaam
Akizungumza katika mahojiano maalum na FullshangweBlog, leo Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe, amesema maandalizi na ukarabati ambao utaendana na hadhi ya mkutano huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa AICC ambao wamejitoa kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi zaidi.
“Kikubwa zaidi ni kuendelea kuwapa morali wafanyakazi na kuendelea kuwahimiza kwamba katika ugeni huu lazima Tanzania iwe kivutio kwa kuhakikisha tunatoa huduma bora hapa ndani.
“Kwa kila mfanyakazi ameishasukwa na kuwekwa sawa kuhakikisha kwamba yupo tayari katika kutoa huduma na kuiletea nchi yetu sifa lakini na Mh. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndio mwenyeji wa mkutano huu mkubwa vile vile naye anapata heshima mbele ya hawa viongozi wageni wake.
“Lazima tujenge jina la nchi kupitia mkutano huu kwa sababu ni mkutano wa tofauti, kwa wenzangu ambao wamenitangulia kuna stori ambazo nazisikia inawezekana kwamba katika mikutano miwili iliyopita, huu ukiwa mkubwa zaidi na mingine iliyofanyika miaka mingi huko nyuma.
“Sasa matamanio yangu ni kwamba kama nchi na taasisi yetu ya AICC pamoja na taasisi nyinge ambazo zipo hapa katika kushughulika na jambo hili, sisi sote tuweze ku’shine’ kwa pamoja kwa ajili ya masilahi mapana ya nchi yetu ya Tanzania,”amesema Bi. Mwakatobe.
Aidha, Bi. Mwakatobe amempongeza Rais Samia kwa kufanya jambo la kijasiri ambalo limeiletea nchi heshima kubwa Kitaifa na Kimataifa.
“Rais ameiheshimisha nchi yetu ya Tanzania, kuifungua nchi sio kitu kidogo na sio kila mtu anaweza kufanya jambo hilo naamini serikali imepitia mikakati mikubwa sana kuifungulia nchi yetu.
“Hivi sasa tunaona kabisa kwenye utalii wa mikutano, mikutano ni mingi sana, mimi nikiangalia kuanzia Julai kwa mfano tarehe moja tulivyoanza mwaka huu wa fedha hadi tarehe 31 Desemba tumekuwa na mikutano 19 ya Kimataifa kati ya Ukumbi wa AICC na JNICC na ya ndani ni mikutano 218,”amesema Bi. Mwakatobe.
Bi. Mwakatobe, amesema kwa hiyo anaiona Tanzania kwa sasa ikiwa imechangamka hadi kutambulika na wageni ambao baadhi wapo tayari kuja Tanzania.
“Kwa hiyo sisi wasaidizi wa Mh. Rais tunatakiwa kutafsri kazi alizozifanya kwa vitendo kwa kuhakikisha kwamba sisi tunafanya wajibu wetu ambao tumepewa ili basi Tanzania yetu iendelee ‘ku’shine’ mbele ya jumuia ya kimataifa.
“Wageni waje, wawekezaji waje, wafanyabiashara wakubwa waje na Watanzania tunufaike na wageni hao, naamini mengi yapo na tunaendelea kunufaika hata kwenye sekta ya utalii nako pia mambo yapo sawa,”alisema Bi. Mwakatobe.