Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Jeshi la Polisi Mkoani Pwani limewakamata watu watatu wanaodaiwa walimchukua mtoto wa miezi saba, Merysiana Melkizedeck, katika tukio la uvamizi lililotokea Januari 15, 2025, ambao walikuwa wamejificha katika msitu uliopo kati ya eneo la Kimalamisale na Serengeti B, kata ya Dutumi, Mlandizi, Mkoani Pwani.
Wahusika wamekamatwa huku mtoto akiwa hai, pamoja na gari T 331 DLZ aina ya Toyota IST, ambalo lilikuwa limeibwa katika uvamizi huo.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Salim Morcase, alieleza kuwa wahalifu hao walikamatwa usiku wa kuamkia Januari 24, 2025.
Aliendelea kusema kuwa, baada ya kumtoa mtoto kutoka kwa wahalifu, walimpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi zaidi, kisha kumkabidhi kwa wazazi wake akiwa salama.
Kamanda Morcase alifafanua kuwa taratibu za upelelezi zinaendelea, ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano ya kina na kumsaka mtuhumiwa mwingine mmoja ambapo baada ya uchunguzi wahusika watafikishwa mahakamani.
” Mnamo Januari 15 mwaka huu, watuhumiwa walivamia nyumba ya Melizedeck Sostenes (28) na mkewe Joan Gabriel, huko Galagaza, Msangani, alifungwa kwa kamba na kutupwa kwenye shimo la choo ambalo lilikuwa halitumiki.”
Kamanda Morcase alitoa wito kwa jamii kutoa taarifa wanapobaini uhalifu na kuwafichua wahusika kwa vyombo vya dola, ili hatua madhubuti ziweze kuchukuliwa.