Mkuu wa mko wa Arusha ,Paul Makonda akizungumza na Mkurugenzi wa Nchi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women), Hodan Addou mkoani Arusha
Mkurugenzi wa Nchi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women), Hodan Addou akizunvumza katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Arusha.
………….
Happy Lazaro, Arusha .
Mkurugenzi wa Nchi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women), Hodan Addou, amefanya ziara Mkoani Arusha ambapo amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, kujadili masuala muhimu yanayohusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika masuala ya kiuchumi.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa. Makonda amesema kuwa, Mkoa wa Arusha umekuwa ukiendesha shughuli za kuwawezesha wanawake kiuchumi sambamba na kuzuia masuala ya ukatili wa Kijinsia kwa wanawake na Watoto na uhamasishaji wa wanawake kushiriki katika masuala ya Uongozi wa ngazi mbalimbali.
Makonda ameongeza kuwa, Kupitia Mradi wa UN WOMEN ujulikanao kama WLER “Strengthening Women And Girls’ Meaningful Participation, Leadership, And Economic Rights”. Ulionufaisha Halmashauri tatu (3) za Mkoa wa Arusha wanawake wamekuwa wakipatiwa elimu kuhusu masuala ya kiuchumi na kutojihusisha na mikopo umiza badala yake kutumia fursa ya Mikopo isiyo na riba ya 10% inayotolewa kwenye Halmashauri zote Nchini.
“Tuna dhamira ya kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wa Arusha wanapewa nafasi za kiuchumi, kijamii, na elimu. Tunaamini kuwa kwa kushirikiana na UN Women, tunaweza kufanya mabadiliko makubwa,” amesema Makonda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Hodan Addou amesema kuwa UN Women imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha kuwa wanawake wanapata nafasi sawa katika sekta zote za maendeleo na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana katika mipango ya maendeleo jumuishi inayozingatia mahitaji ya wanawake vijijini na wale walioko katika mazingira magumu.
“Uwezeshaji wa wanawake si tu suala la haki za binadamu bali ni msingi wa maendeleo endelevu na tunafurahi kuona Mkoa wa Arusha ukichukua hatua madhubuti katika kusimamia usawa wa kijinsia,” amesema Addou.