Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussi Khamis Debe, amesema ushirikiano baina ya Taasisi za Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zinazofanana katika majukumu umesaidia kuimarisha utendaji kazi wa Taasisi hizo, hasa katika kuwahudumia watu wenye ulemavu.
Debe alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha mashirikiano kati ya watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulema
Akizungumza katika kikao hicho, Debe alisema mashirikiano hayo yamewezesha kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuwahudumia watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ushirikishwaji wao katika masuala ya ajira, afya, elimu, na mafunzo ya uwezeshaji kiuchumi. Pia, alisisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati wa kitaifa utakaoongoza sekta mbalimbali kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu na kuwapa kipaumbele.
“Mashirikiano kama haya yanazisaidia taasisi pacha kubadilishana uwezo na uzoefu katika kutekeleza majukumu yao,” alisema Debe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Rasheed Maftah, alieleza kuwa mashirikiano hayo yamewezesha kuandaa mradi wa teknolojia saidizi kwa watoto wenye ulemavu, pamoja na kutoa maono ya uanzishwaji wa kozi ya malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya watoto wenye ulemavu katika Chuo Kikuu cha Aga Khan.
Maftah aliongeza kuwa hatua hizo pia zimeboresha mfumo wa taarifa za watu wenye ulemavu ngazi ya kaya, kutungwa kwa Sheria mpya ya Watu Wenye Ulemavu Na.8 ya mwaka 2022, na kanuni zake za mwaka 2023 kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, mwanafunzi mmoja mwenye ulemavu kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja amepewa nafasi ya kusoma katika Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu Yombo, hatua ambayo ni sehemu ya juhudi za mashirikiano hayo.
Ofisa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu kutoka Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Zeyana Ahmed Kassim, alisema ushirikiano huo umefanikiwa kuunda mfumo wa pamoja wa kuratibu masuala yote ya utengamao kwa watu wenye ulemavu. Aliongeza kuwa mashirikiano hayo yanatengeneza kundi lenye sauti moja la kutetea haki za watu wenye ulemavu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zeyana alihitimisha kwa kusema kuwa taasisi hizo zitaendelea kushirikiana katika kufanya tafiti, kuandika miradi, na kujenga mahusiano ya kimataifa ili kuhakikisha fursa sawa kwa watu wote wenye ulemavu.