Na Fauzia Mussa
Vijana wametakiwa kutumia fursa za kielimu ili kuboresha mustakabali wao na kujiandaa kwa nafasi za kujiajiri.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Taasisi ya Yunus Emre Zanzibar, Ibrahim Kubilay, wakati akizungumza na vijana waliojiunga na taasisi hiyo iliyopo Kibele, Mkoa wa Kusini Unguja.
Kubilay alieleza kuwa Taasisi ya Yunus Emre imejikita katika kufundisha lugha ya Kituruki na tamaduni zake kwa lengo la kujenga uhusiano wa karibu na kutanua fursa za kimataifa.
“Taasisi ya Yunus Emre inatoa mafunzo ya lugha ya Kituruki bila malipo katika nchi mbalimbali. Mpaka sasa ina vituo 92 katika nchi 68, ikiwa na lengo la kukuza uhusiano wa kimataifa na fursa za mawasiliano,” alisema Kubilay.
Aliongeza kuwa mbali na mafunzo ya lugha, taasisi hiyo pia huwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza utamaduni wa Kituruki kupitia michezo, vyakula, mavazi, na matukio maalum ya kitamaduni yanayoandaliwa kwa ajili ya kueneza na kuurithisha utamaduni huo kwa jamii mbalimbali.
Kubilay pia alieleza kuwa kituo hicho kinadumisha mahusiano ya kiutamaduni kwa kuwapatia vijana wa Zanzibar nafasi ya kutembelea Uturuki na kuwakaribisha vijana wa Kituruki kuja Zanzibar. “Hii inatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha uhusiano wa kimataifa,” aliongeza.
Wanafunzi wanaosoma katika darasa la lugha ya Kituruki walielezea faida za kujifunza lugha za kigeni. Haji Foum Juma alisema kujifunza lugha za kigeni huongeza uwezo wa mawasiliano, ufanisi kitaaluma, na nafasi za kusafiri.
“Kujiunga na madarasa kama haya si tu kunatuwezesha kujifunza lugha za kigeni, bali pia kunapanua upeo wa kujua tamaduni mpya na kutengeneza mahusiano mapya yenye manufaa,” alisema Haji.
Aidha, aliongeza kuwa baada ya kuhitimu, anatarajia kutumia maarifa hayo kujiajiri katika sekta ya utalii au kufungua darasa la kufundisha vijana wengine.
Arafa Shaibu Ismaili aliwasihi vijana wenzake kuchangamkia fursa kama hizo kwa sababu zinawasaidia kujiajiri na kuepuka utegemezi kwa familia na Taifa kwa ujumla.
Mhitimu wa darasa hilo, Amina Daudi, alisema amenufaika na mafunzo hayo kwani sasa anatumika na taasisi hiyo kama mtafsiri wa lugha ya Kituruki kwa wageni wanaotembelea Zanzibar.
Taasisi ya Yunus Emre imeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya vijana kwa kutoa mafunzo na fursa za kiutamaduni zinazochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.