Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia, na Habari, Jerry Silaa, amesema kuwa serikali imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaounganisha Tanzania na Kenya kupitia Horohoro hadi Mombasa, Kenya. Mkongo huo pia umeunganishwa na mikongo ya mawasiliano ya chini ya bahari kupitia Dar es Salaam.
Akizungumza Januari 23, 2025, wakati wa ziara ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika eneo la Horohoro, mpakani mwa Tanzania na Kenya, Waziri Silaa alisema Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni mtandao mkubwa wa nyaya za mkongo unaounganisha maeneo mbalimbali ya nchi kupitia NICTBB.
“Tunazo kilomita 13,991 za mkongo, na lengo letu kufikia kilomita 15,000 ifikapo Juni mwaka huu. Hii inawezekana kutokana na uwezeshaji mkubwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na juhudi za wizara katika kuimarisha TTCL,” alisema Silaa.
Aidha, Waziri Silaa alibainisha kuwa mkongo huo umefanikiwa kuunganisha wilaya 109 kati ya wilaya 139 za Tanzania, huku zabuni zikitangazwa na bajeti ya mwaka 2024-2025 ikitenga fedha kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kuunganisha wilaya zilizobaki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema kuwa kilomita 13,991 za mkongo zimekwishajengwa na zinaunganisha Tanzania Bara na nchi jirani, zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, na Malawi.
“Mradi huu siyo tu unaimarisha mawasiliano ya ndani bali pia unasaidia kuunganisha Tanzania na nchi jirani. Kupitia mkongo wa Mombasa, tunaongeza njia mbadala kwa mikongo ya Dar es Salaam, ambapo sasa tutakuwa na uwezo wa kutumia mikongo saba zaidi,” alisema Marwa.
Aliongeza kuwa mradi huu unapanua uwezo wa kusafirisha data, jambo ambalo litasaidia maendeleo ya teknolojia na biashara ndani na nje ya nchi. Marwa alihitimisha kwa kusema kuwa mradi huo unatarajiwa kuanza kazi rasmi ifikapo Februari 1, 2025.