DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
Marais 25 wa Nchi za Afrika, pamoja na Mawaziri wa Fedha na Nishati zaidi ya 60, wanatarajiwa kushiriki Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliopangwa kufanyika Januari 27-28, 2025, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo unalenga kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo kusaini mkataba wa kuwezesha kusambaza umeme kwa watu milioni 300 kabla ya mwaka 2030.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano huo, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeshughulikia masuala ya Nishati na Mabadiliko ya Hali ya Hewa, Dkt. Kevin Kariuki, alisema kuwa mkutano huo utawashirikisha marais 25 wa mataifa ya Afrika na mawaziri zaidi ya 60 wa fedha na nishati.
Kwa mujibu wa Dkt. Kariuki, viongozi kutoka mataifa mengine ya nje pia watashiriki kama mashuhuda wa hatua ya marais hao kusaini mkataba muhimu wa kuwezesha upatikanaji wa nishati kwa watu milioni 300 kufikia mwaka 2030.
“Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Rais wa Benki ya Dunia walikubaliana Aprili 2024 kwamba ulimwengu hauwezi kuendelea kuishi na upungufu wa nishati ya umeme. Hivyo, mipango ya kuhakikisha nishati inasambazwa kwa watu milioni 300 kabla ya mwaka 2030 itajadiliwa kwa kina,” alisema Dkt. Kariuki.
Aidha, Dkt. Kariuki aliongeza kuwa mkutano huo utahusisha pia kusainiwa kwa mkataba unaoonesha mikakati ya kupunguza ukosefu wa huduma ya nishati ya umeme barani Afrika.