Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) umefanya semina kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kushirikiana na vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa matano muhimu ambayo hayakuwa yanapewa kipaumbele nchini.
Mafunzo hayo ni hatua kubwa katika kuimarisha juhudi za kuelimisha umma kuhusu magonjwa ya matende na mabusha, trakoma, usubi, minyoo ya tumbo, na kichocho, ambayo bado ni changamoto kwa baadhi ya maeneo nchini licha ya juhudi za serikali na wadau wa afya.
Akizungumza wakati wa kufungua semina hiyo, Kaimu Meneja wa Mpango huo, Dkt. Faraja Lyamuya, alibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi ya magonjwa hayo. Halmashauri 114 ambazo awali zilikumbwa na ugonjwa wa matende na mabusha sasa zimeacha kugawa kingatiba kutokana na maambukizi kushuka chini ya asilimia mbili.
Dkt. Lyamuya alisisitiza kuwa, imani potofu zinazohusisha magonjwa haya na mila au uchawi ni changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo. Alieleza kuwa ugonjwa wa matende na mabusha hauhusiani na ulaji wa madafu wala uchawi, bali unasababishwa na mbu wanaobeba vimelea.
Kwa upande wake, Dkt. Lilian Ryatura, Afisa wa Mpango huo, alisema kuwa maambukizi ya trakoma yameshuka kutoka halmashauri 69 zenye maambukizi ya juu hadi tisa pekee, kutokana na matumizi ya kingatiba ya Zithromax.
Magonjwa ya kichocho, minyoo ya tumbo, na usubi pia yalijadiliwa katika semina hiyo, ambapo wataalamu waliwataka wananchi kutilia mkazo matumizi ya kingatiba na kufuata ushauri wa afya ili kujikinga na madhara makubwa kama vile utapiamlo, udumavu, na matatizo ya damu.
Dkt. Mohamed Nyati aliitaka jamii kuepuka tabia hatarishi kama kufua na kuogelea kwenye maji yaliyotuama, huku Afisa Mpango Ruth Mchomvu akitoa wito kwa watu walio katika maeneo yenye hatari kubwa ya maambukizi kumeza kingatiba za usubi bila kusubiri dalili.
Mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani, inayotarajiwa kufanyika Januari 30. Mwaka huu, maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu: “Tuungane. Tuchukue Hatua. Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.”
Kwa kushirikiana na vyombo vya habari, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele umeweka msingi wa kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wote ili kuimarisha afya ya jamii na kupunguza mzigo wa magonjwa haya nchini.