Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw. James Kaji akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu zoezi la ukusanyaji vitambulisho vya Taifa kutoka Ofisi za Kata, Vijijini na Mitaa na Uchukuaji wa vitambulisho.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw. Geoffrey Tengeneza akizungumza jambo katika mkutano wa waandishi wa habari leo Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wakitoa taarifa kuhusu zoezi la ukusanyaji vitambulisho vya Taifa kutoka Ofisi za Kata, Vijijini na Mitaa na Uchukuaji wa vitambulisho.
……………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewataka wananchi walitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kufika kwa wakati katika Ofisi za NIDA za Wilaya walikosajiliwa kwa ajili ya kuchukua vitambulisho vyao ndani ya muda ulioainishwa ili kuepuka matumizi ya namba zao za utambulisho wa Taifa (NIN) kusitishwa.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Bashungwa ambapo Disemba 17, 2024 alitoa maagizo kwa NIDA kuhakikisha ndani ya miezi miwili vitambulisho vyote 1, 200,000 vilivyokuwa ofisi za kata, Vijiji, Mitaa, Vitongoji viwe vimegawiwa na kuchukuliwa na wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw. James Kaji amesema kuwa wameamua kukusanya vitambulisho vyote vilivyokuwa katika ofisi za kata, Vijiji, Mitaa, Vitongoji nchini zote kote na kuvirudisha katika ofisi za Wilaya za NIDA.
Bw. Kaji amesisitiza kuwa maelekezo yaliyotolewa ya kusitisha matumizi ya namba ya utambulisho ni wale ambao wamepata ujumbe mfupi wa maandishi halafu wakaacha kujitokeza kwenda kuchukua vitambulisho vyao, huku akieleza kuwa kama mtu hujapata sms ya kumjulisha kitambulisho chake kipo Ofisi za NIDA za Wilaya fulani namba yake haitazuiwa.
“Ujumbe mfupi wa sms ambao tumekuwa tukiwatumia wahusika wa vitambulisho ambavyo havijachukuliwa pamoja na mambo mengine unasema kwamba asipofika kuchukua kitambulisho chake ndani ya muda ulioelekezwa matumizi ya namba yake ya utambulisho wa Taifa (NIN) yatasitishwa” amesema Bw. Kaji.
Bw. Kaji amesema kuwa ili kufikia malengo wameuganisha mfumo wa NIDA NA TCRA ili kuwezesha NIDA kutuma SMS kwa namba ya simu iliyosajiliwa kwa kutumia namba ya Kitambulisho ya mwananchi inayotumika kwa sasa.
Amesema kuwa baadhi ya wananchi ambao wakati wanasajiliwa walikuwa mahali tofauti na wanapoishi sasa, wameruhusu mtu kumchukulia kitambulisho cha ndugu au jamaa yake akiwa na sms aliyetumiwa ya kwenda kuchukua kitambulisho hicho.
Bw. Kaji amefafanua kuwa kwa mujibu wa utafiti waliofanya kuhusu wananchi kushindwa kuchukua vitambulisho vyao umebaini baadhi yao kutokujali kuchukua vitambulisho kwa kuwa namba za utambulisho wanayo, hivyo wanapata huduma zote sawa na wenye kitambulisho pale inapohitajika huduma zenye sharti la kuwa na Kitambulisho cha Taifa au Namba.
Amesema sababu nyengine ni baadhi ya wananchi kuhama kutoka sehemu waliyokuwa wanaishi wakati wanajisajili ambako ndiko vitambulisho vyao vimepelekwa na kwenda sehemu nyengine pamoja na baadhi ya wananchi kufariki.
Katika hatua nyengine amefafanua kuwa wananchi wenye vitambulisho vyenye changamoto ikiwemo kufutika maandishi kuvirudisha katika ofisi za NIDA za Wilaya, Kata, Vijiji na Mitaa na kutengenezewa kitambulisho kipya bila malipo yoyote.
Amesema kuwa mpaka sasa jumla ya vitambulisho 31,000 vilivyokuwa vimefutika vimepokelewa na kuchapishwa upya na kugawiwa kwa wahusika, huku akieleza kuwa NIDA inaendelea kukusanya vitambulisho vyote vyenye changamoto kwa ajili ya kuvichapisha tena.