Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Ziwa Imelda Banali akizungumza kwenye semina ya wahariri,waandishi na watangazaji wa vyombo mbalimbali Jijini Mwanza
………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkoa wa Mwanza umetajwa kuwa Mkoa wa pili Kitaifa kwakuwa na idadi kubwa ya laini za simu hatua inayopelekea kuchochea ongezeko la uchumi.
Hayo yameelezwa Leo Jumanne Januari 21, 2025 na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Ziwa (TCRA), Mhandisi Imelda Banali wakati alipokuwa akifungua semina ya wahariri,waandishi na watangazaji wa vyombo mbalimbali vya habari Jijini Mwanza.
Semina hiyo ilikuwa na mada ya kutoa taarifa za mwenendo wa sekta ya mawasiliano kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha Oktoba hadi Disemba 2024/2025.
Amesema kuwepo kwa idadi kubwa ya huduma za mawasiliano mkoani hapa ni fursa kubwa kwa watu wanaoanzisha biashara.
“Kama unaanzisha biashara ambayo itategemea mitandao kwaajili ya kuwafikia wateja wako utakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya biashara nzuri kwani idadi ya laini za simu zilizopo kwenye mkoa wetu wa Mwanza ni kubwa sana”, amesema
Aidha, amewatahadharisha wananchi kuwa makini kwenye matumizi ya mitandao kwani pamoja na kuwepo kwa idadi nyingi za laini za simu ambazo zimesajiliwa kunaweza kukawavutia watu wanaotumia vibaya huduma za mawasiliano kwa kufanya utapeli.
Pia aliwaomba wanahabari kutumia Kalam zao kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuelewa vitu vinavyofanywa na serikali kupitia sekta ya mawasiliano.
Akiwasilisha ripoti ya Sekta ya Mawasiliano kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha Oktoba hadi Desemba 2024/2025, Mkurugenzo wa Masuala ya Kisekta Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Mwesigwa Felician amesema kwenye robo hiyo kumekuwepo na ongezeko kubwa la huduma za mawasiliano ambazo zinachochea fursa mbalinbali zinazoweza zikatumiwa na wananchi.
Amesema uharifu wa mtandaoni umepungua kwa asilimia 19 kutoka 19000 hadi 12000 kwenye robo hii ya pili.
“Ripoti imeonesha Mikoa ambayo matatizo ya ulaghai kwenye mitandao bado ni changamoto ni Rukwa na Morogoro hususani Wilaya ya Kilombelo na Sumbawanga,”