Kwa mwaka wa nane mfululizo, kampuni ya Vodacom Tanzania PLC imethibitishwa kuwa Mwajiri Bora na Taasisi ya Waajiri Bora (Top Employer Institution) huku ikishika nafasi ya kwanza nchini kwa mwaka 2025. Utambuzi huu wa heshima na nafasi ya kwanza miongoni mwa Waajiri Bora waliothibitishwa pia imetolewa kwa kundi la Makampuni ya Vodacom barani Afrika (Vodacom Group), Vodacom Afrika Kusini, Vodacom Msumbiji na Safaricom Kenya.
Mwaka 2024, Vodacom iliboresha programu yake ya kuongeza thamani kwa Wafanyakazi wake kwa kuongeza huduma zinazothibitisha adhma yake ya kuunda mazingira ya kazi jumuishi. Kwa kutilia mkazo mafunzo na maendeleo ya ujuzi, ushirikishwaji wa wafanyakazi, sera thabiti za likizo na utamaduni mzuri wa kazi, Vodacom imeendelea kuonesha njia katika nyanja ya mahusiano ya wafanyakazi nchini.
“Kudumisha nafasi yetu kama Mwajiri Bora hapa nchini, kunadhihirisha ari yetu ya kuwawezesha wafanyakazi wetu kufanya kazi kwa bidii. Tumeweka kipaumbele kwenye kuwafanya wafanyakazi wetu wajisikie kuthaminiwa kwa kutoa faida mbalimbali kwao na familia zao, kukuza vipaji vya vijana kupitia mpango wetu wa mafunzo ya Wahitimu (Graduate Trainee) miongoni mwa mipango mingine, kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika teknolojia kupitia programu yetu ya Code Like a Girl kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 – 18 na hivi karibuni, tulianzisha Kituo cha kuongeza ujuzi wa Kidigitali kinachotoa mafunzo kwa njia ya mtandao kwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 ambao ni mustakabali wa kazi katika uchumi wa kidigitali unaokua kwa kasi,” anasema Vivienne Penessis, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa kampuni hiyo.
Taasisi ya Waajiri Bora inatoa tuzo hii kwa kampuni kulingana na utendaji wao katika maeneo muhimu ya rasilimali watu kama vile mkakati wa wafanyakazi, mazingira ya kazi, upatikanaji wa vipaji, kujifunza, na ustawi. Kutokana na mashirika mengi zaidi ya Tanzania kushiriki katika uthibitisho wa Mwajiri Bora kwa mwaka 2025, taasisi hiyo imeweza kuzipa alama kampuni hizo kulingana na vigezo vilivyowekwa na hivyo kuitambua Vodacom Tanzania kama Mwajiri Bora nambari 1 nchini.
“Kwa miaka 8 mfululizo tumekuwa tukiorodheshwa kama Mwajiri Bora lakini kutajwa kuwa nambari 1 nchini kwa mwaka huu ni jambo la kusisimua. Kama shirika, jitihada zetu zakibunifu zinakwenda zaidi ya jinsi tunavyobuni na kutoa bidhaa na huduma zetu hadi jinsi tunavyowajali wafanyakazi wetu na kujenga nguvukazi itakayochangia kikamilifu katika ukuaji na maendeleo ya Tanzania. Kama Mwajiri Bora, tutaendelea kutoa fursa ndani na nje ya Vodacom, kukuza mazingira mazuri ya kazi na kuwawezesha wafanyakazi wetu kuwa na usawa kati ya kazi na maisha yao binafsi,” alisema Philip Besiimire, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.