Octavian Mshiu, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) akizungumzia mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Nishati.
DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
Octavian Mshiu, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), amefanya mahojiano maalum kuhusu tukio kubwa linalosubiriwa kwa hamu nchini Tanzania yaani Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu nishati pamoja na wadau wa maendeleo, utakaofanyika Januari 27 na 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.
Akizungumza kwa utulivu katika mahojiano hayo, mawazo yake yalirudia kile ambacho mkutano huo unawakilisha: mustakabali wa nishati barani Afrika. “Huu si mkutano wa kawaida,” alisema Mshiu akionesha kutafakari athari chanya ambazo Tanzania na Afrika kwa ujumla zinaweza kuvuna.
Ni wazi mkutano huu utajadili masuala mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Nishati ikiwemo vyanzo vya nishati mbadala kama vile upepo, jua, na maji.Upanuzi wa upatikanaji wa umeme vijijini na mijini, kuhakikisha nishati inawafikia watu wengi zaidi barani Afrika ikiwa ni pamoja na Uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kulinda afya ya umma na mazingira.
“Majadiliano haya yatafungua milango ya fursa ikiwemo sekta binafsi hasa kwa wanachama wetu wa TPSF ambao moja kwa moja wapo katika sekta ya nishati, kampuni kubwa zinazohusika na nishati na wajasiriamali wadogo kwa ujumla wake ,” alisema akisisitiza kuwa kila kila mdau ana nafasi yake kwenye ajenda ya mkutano huo.
Kwa uchangamfu, Mshiu alizungumza kuhusu nafasi ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Alimsifu kwa kuweka mkazo mkubwa katika nishati safi na maendeleo endelevu.
“Tangu Rais Samia aingie madarakani, ameweka msingi imara wa utalii wa mikutano na miradi ya kimkakati. Ni jambo la kujivunia kuwa taifa letu ni mwenyeji wa tukio hili kubwa ambalo litaiweka Tanzania mbele katika mazungumzo ya nishati barani Afrika,” alisema Mshiu.
Kwa Mshiu, juhudi za Rais Samia zimeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika, hususan katika kupigania suluhisho endelevu la nishati safi.
Akizungumzia jamii za vijijini na sekta ya misitu, Mshiu alionesha matumaini makubwa kwa fursa zinazokuja. Alisema vijiji vinavyotunza misitu vina nafasi ya kujifunza jinsi ya kuingia kwenye matumizi ya Nishati safi na kunufaika kiuchumi kutokana na ulinzi wa mazingira hasa misitu.
Aidha, alitoa mwito kwa kampuni za gesi kutumia mkutano huo kuimarisha mbinu za masoko yao hasa katika jamii za vijijini.
Katika mahojiano yake, Mshiu aligusia pia ongezeko la matumizi ya gesi kwa magari nchini hasa jijini Dar es Salaam.
Alisema biashara hiyo imekuwa suluhisho la gharama nafuu na safi kwa wamiliki wa magari huku ikiyalinda mazingira kwa kuacha hali ya hewa ikiwa safi.
“Hivi sasa, tunaona vituo vya gesi vikihudumia magari mengi zaidi. Wafanyabiashara wa sekta hii hawapaswi kupuuza nafasi hii ya mkutano wa Nishati ili kujifunza na kushirikiana na wadau wengine katika kuongeza uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi,” alisema, akiwahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa magari kuangalia fursa zilizopo kwenye nishati safi.
Ujumbe wa Mshiu ulikuwa dhahiri: Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati Safi ni fursa ya kipekee kwa Tanzania na bara zima la Afrika