Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi,
…………..
Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umetoa uamuzi mzito kwa kauli moja, kumuidhinisha Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea urais wa Tanzania Bara katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Vilevile, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameidhinishwa kuwa mgombea wa urais Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho.
Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kwa kura nyingi za wajumbe ambapo alichaguliwa kww asilimi mia moja sawa na kura 1924 za wajumbe wote.
Wajumbe wa mkutano huo wameeleza kuwa maazimio haya yanatokana na kazi nzuri iliyofanywa na viongozi hao katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo imeleta mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo. Wajumbe walisisitiza umuhimu wa kutangazwa mapema kwa wagombea ili kuimarisha maandalizi ya chama kuelekea uchaguzi.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, aliwaeleza wajumbe kuwa uamuzi wa kuridhia maazimio haya ni jukumu lao. Alisema kuwa hatua hii inapaswa kufanyika kwa utaratibu wa kisheria ili kuhakikisha hakutakuwa na mgongano wa kikatiba au kisheria.
Aidha, Dkt. Kikwete alisisitiza kuwa hatua ya kutangaza mapema wagombea wa nafasi za juu za uongozi si jambo lenye changamoto kubwa, bali ni njia ya kuimarisha mshikamano ndani ya chama.
Kwa upande wake, Dkt. Kikwete aliongeza kuwa CCM itaibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa 2025 kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya Watanzania moja kwa moja. Alisema, “Serikali zote mbili za Muungano na Zanzibar zimefanya kazi kubwa ambayo imejenga imani kwa wananchi.”
Uamuzi huu wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM umeonyesha mshikamano wa chama hicho na nia ya kuendelea kuwatumikia wananchi kupitia viongozi waliopo madarakani.