Wekundu wa Msimbazi Simba SC imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika Kundi A Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya CS Constantine katika mchezo uliochezwa leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba SC imefanikiwa kupata mabao kipindi cha pili kupitia kwa Kibu Denis na Leonel Ateba, huku wakihakikisha wanamaliza kwa pointi moja mbele ya wapinzani wao wa Algeria kwenye kilele cha kundi hilo.
Denis amefunga bao kwa mkwaju mkali kutoka ndani ya eneo la goli, kabla ya Ateba kumaliza kabisa baada ya shambulizi la kushtukiza kuhitimisha matokeo zikiwa zimesalia dakika 11.
Timu zote mbili zimefuzu kwa robo fainali, huku Simba ikijikusanyia pointi 13 kutoka kwenye kampeni za kundi hilo huku Constantine akiambulia nafasi ya pili kwa pointi 12.
Wakati huo huo katika mchezo mwingine wa kundi hilo, CS Sfaxien imefanikiwa kupata ushindi mnono mabao 4-0 dhidi ya Bravos do Maquis.
Timu hiyo ya Tunisia ikiondoka kwenye Kombe la Shirikisho la CAF ikiwa na pointi tatu pekee kutoka kwa kampeni ya kundi.
Licha ya kuonyesha uhodari wao wa kushambulia katika mechi hii ya mwisho ya kundi, CS Sfaxien wamemaliza katika kundi A wakiwa wameshika mkia.