NA FAUZIA MUSSA
BALOZI wa Vijana Zanzibar, Mohammed Kassim Mohammed, maarufu kama Prince Eddycool, amewahimiza vijana kuwa wabunifu na kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kujiajiri na kujiongezea kipato.
Akizungumza wakati alipotembelea miradi ya kilimo ya vijana wa Baraza la Vijana Shehiya ya Miwani, Wilaya ya Kati, Prince Eddycool alisema Serikali inatoa msaada mkubwa kwa miradi ya vijana, hivyo ni muda muafaka wa kuchangamkia fursa hizo.
“Vijana mna vipaji vingi, na iwapo mtatumia vipaji hivyo kwa bidii, mtaweza kuanzisha miradi yenu na hata kuwaajiri wengine,” alisema.
Pia, alisisitiza kuwa Zanzibar ina ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo na kwamba ikiwa vijana wataitumia vyema, watafanikiwa kwa kiasi kikubwa. “Kijiji chetu kina ardhi nzuri kwa kilimo. Mkitumia fursa hizi kwa umakini, mtafanikiwa kufika mbali katika maisha yenu,” aliongeza.
Aidha, alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zake za kuwezesha maendeleo ya vijana na kuonyesha kuwa Serikali inaunga mkono juhudi za kujiajiri na kuajiri wengine.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Shehiya ya Miwani, Seif Hassan Seif, alielezea kuwa jumla ya vijana 35 wamekusanyika kuendeleza kilimo cha bamia na muhogo ili kujikwamua kimaisha na kuondokana na utegemezi wa familia zao na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, alibainisha changamoto kama ukosefu wa ardhi ya kudumu na tatizo la maji, kwani wanategemea mito ambayo hukauka hasa wakati wa kiangazi. “Eneo tunalolitumia si letu. Wakati wowote tunaweza kuondolewa endapo mmiliki atahitaji kutumia ardhi hiyo kwa shughuli nyingine,” alisema Seif.
Kwa upande wake, Zainab Salum Ahmad, mmoja wa wanachama wa baraza hilo, alitoa wito kwa wanawake kujitahidi kiuchumi badala ya kutegemea familia au waume zao. Alisisitiza kuwa jitihada na mshikamano vitatoa manufaa kupitia miradi ya kilimo, kama ilivyokuwa kwa miradi mingine ya mahindi hapo awali.