Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini Mhandisi Florence Mwakasege (wa kwanza kushoto) akitoa maelekezo kwa fundi umeme leo Januari 17, 2025, Dar es Salaam akiwa katika ziara ya kukagua utengenezaji wa miundombinu ya umeme katika Kata ya Kimara baada nguzo ya umeme kuanguka katika barabara ya njia panda ya malamba mawili.
Picha za matukio mbalimbali za mafundi umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini wakiendelea na matengenezo ya miundombinu ya umeme katika Kata ya Kimara, Dar es Salaam
……..
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini Mhandisi Florence Mwakasege leo Januari 17, 2025 amefanya ziara ya kukagua utengenezaji wa miundombinu ya umeme katika Kata ya Kimara baada nguzo ya umeme kuanguka katika barabara ya njia panda ya malamba mawili.
Nguzo hiyo imeanguka baada ya gari kubwa kuvuta nyaya ya umeme hali ambayo imesababisha baadhi ya wateja katika eneo hilo kukosa huduma ya umeme kwa muda.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Meneja TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini Mhandisi Florence Mwakasege, amesema kuwa taarifa ya tukio la kuanguka kwa nguzo wamepata leo majira ya saa tano asubuhi , huku akieleza kuwa tayari timu ya mafundi umeme wamefika eneo la tukio kurekebisha hitilafu hiyo haraka ili kurudisha huduma ya umeme.
Mhandisi Mwakasege amekagua hatua zilizochukuliwa na mafundi na kuhakikisha matengenezo yanafanyika kwa usahihi na haraka ili kuzuia usumbufu kwa wateja.
“Natoa rai kwa wananchi kutoa taarifa mapema kwa TANESCO kwa wakati inatokea hitilafu ya umeme kupitia namba ya huduma kwa wateja 0756 251 753, pia kuwa makini wakati wanapita karibu na miundombinu ya umeme ili kuepuka kusabaisha kero kwa wateja” amesema Mwakasege.