Kiteto, Januari 14, 2025
Afisa Misitu wa Jumuiya ya Uhifadhi Msitu wa SULEDO, Bw. Siloma Manyindo Mtero, amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Kiteto kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 600,000.
Mashtaka hayo yamefunguliwa chini ya Kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, kama ilivyorekebishwa mwaka 2022, pamoja na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu chini ya Kifungu cha 302 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.
Kwa mujibu wa mashitaka, Bw. Mtero anatuhumiwa kuomba rushwa hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ndilali ili kuruhusu baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho kufanya shughuli za kilimo ndani ya msitu wa SULEDO, kinyume na sheria za uhifadhi.
Shauri hilo lilisomwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Wakili Yahaya Masakilija, mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Aron Losioki.
Mshtakiwa alikana mashtaka yote yanayomkabili, lakini ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo amepelekwa mahabusu. Shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe 28 Januari 2025 kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali.