Serikali inaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanzisha Mfuko wa Nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameiarifu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira leo Januari 16, 2025 jijini Dodoma, alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyotokana na taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati iliyowasilishwa bungeni Februari, 2024.
Amesema Kanuni za Usimamizi wa miradi ya biashara ya kaboni zimebainisha ruzuku kupitia hakimiliki za kaboni zinazopatikana kutokana na kupunguza matumizi ya nishati inayochafua mazingira, hivyo ruzuku hii ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kutekeleza malengo ya kupunguza gharama kwa watumiji wa nishati safi.
Mhe. Khamisi ameileza kamati hiyo kuwa katika jitihada za kupunguza gharama za matumizi ya nishati mbadala, Serikali imesaini makubaliano ya awali na wawekezaji kuhusu ruzuku ya shilingi bilioni 8.64 kwenye nishati safi ya kupikia mbapo jumla ya majiko 452,455 yamepata ruzuku.
Aidha, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa njia mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, ziara za viongozi.
Kwa upande mwingine amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea
kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kuhamasisha na kuhimiza Halmashauri zote za vijiji kuainisha misitu yote ya vijiji yenye sifa ya kuingizwa kwenye mpango wa Biashara ya Kaboni.
Amefafanua kuwa uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa biashara ya kaboni katika kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato kwa jamii unaendelea kutolewa kwa wananchi ambapo Serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa mikataba ya biashara ya kaboni inanufaisha wananchi na inafanyika kwa mujibu wa Kanuni za usimamizi wa biashara ya kaboni.
Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira inayoongozwa na Mwenyekiti Mhe. Jackson Kiswaga imeipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwakutanisha wadau na kujadili changamoto za mazingira ili kuzipatia ufumbuzi.
Pamoja na hayo imesisitiza elimu ya mazingira iendelee kutolewa ili wananchi waweze kupata uelewa na kuachana na vitendo vya uharibifu wa mazingira vikiwemo uchomaji na ukataji wa miti.
Pia, imesema elimu ya nishati safi ipewe msukumo kwani wananchi wengi hususan wa maeneo ya vijijini hawana uelewa wa umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia hivyo kwa kuwapa elimu wataachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akifafanua hoja amesema hadi kufikia Desemba 30, 2024, maombi ya miradi 65 ya biashara ya kaboni yamepokelewa.
Amefafanua kuwa jumla ya miradi sita imepata barua za kukubaliwa kuanza mchakato wakati miradi sita imetimiza vigezo na hatua za kupatiwa barua inaendelea.