Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dk. Said Seif Mzee, ametoa wito kwa jamii kuunga mkono wajasiriamali wazawa kwa kununua bidhaa zinazozalishwa nchini. Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho ya 11 ya Kitaifa ya Biashara yaliyofanyika katika viwanja vya ZITF, Dimani, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Dk. Said alisisitiza umuhimu wa kuthamini na kutumia bidhaa za ndani ambazo zina ubora wa hali ya juu.
Dk. Said alibainisha kuwa maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kujifunza na kupata uzoefu utakaoboresha ufanisi wa shughuli zao. Aliwahimiza wajasiriamali kuendelea kushiriki katika maonesho hayo ambayo yamekuwa yakiboreshwa kila mwaka.
“Maonesho haya ni fursa ya pekee kwa wajasiriamali kupata maarifa mapya na kuboresha biashara zao. Aidha, matukio mbalimbali yaliyofanyika wakati wa maonesho haya, kama vile Siku ya Sukari, Siku ya Utalii, Siku ya Biashara, Siku ya Leseni, Siku ya Vipimo, na Siku ya Wajasiriamali, yamechangia kuongeza uelewa na ubunifu kwa wajasiriamali,” alisema Dk. Said.
Aidha, aliongeza kuwa maonesho hayo yamefanikiwa kwa kuwahusisha wajasiriamali wa visiwa vya Pemba, na akawataka waendelee kushiriki kwa wingi katika maonesho yajayo ili kuongeza fursa za masoko na mtandao wa kibiashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Biashara na Masoko, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Khamis Ahmad Shauri, alieleza kuwa idadi ya washiriki imeongezeka kutoka 377 mwaka 2024 hadi 438 mwaka 2025. Pia aliahidi kuwa wizara itaendelea kufanya maboresho zaidi ili kuhakikisha maonesho hayo yanavutia washiriki wa ndani na nje ya nchi.
Mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Khamis Issa Mohammed, alitoa shukrani kwa Serikali kwa kuweka jukwaa hilo ambalo limewakutanisha wafanyabiashara na wajasiriamali wa ndani. Aliwahimiza wajasiriamali waliokosa kushiriki mwaka huu kujiandaa kwa maonesho yajayo.
Maonesho hayo, yaliyofunguliwa rasmi Januari 1, 2025, na kufungwa Januari 15, 2025, yalihitimishwa kwa kuwatunuku zawadi na vyeti vya shukrani wadhamini wa maonesho.