Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Katika juhudi za kuimarisha elimu na kuinua maisha ya vijana wilayani Same, Mkuu wa Wilaya, Mhe. Kasilda Mgeni, ametoa wito kwa wasimamizi na mafundi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Amali, iliyopo Kata ya Kihurio, wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kuongeza kasi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Machi 15 mwaka huu kwa kuzingatia viwango na ubora.
Akizungumza na kamati ya ujenzi pamoja na mafundi wakati wa kukagua mradi huo, Mhe. Kasilda amewaagiza mafundi kuongeza kasi ya kufanya kazi usiku na mchana, huku akisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya mafundi, kamati ya ujenzi na halmashauri.
“Fanyeni kazi usiku na mchana. Msisubiri changamoto za vifaa ziwafikie na zipite kimya kimya bila taarifa. Shirikianeni na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kutatua changamoto yoyote inayojitokeza ili kusiwepo na ucheleweshaji wa maendeleo ya mradi huu muhimu,” amesema Mhe. Kasilda.
Pia Mhe. Kasilda amesisitiza kuwa mradi huu una umuhimu wa kipekee kwa jamii ya Same, kwani shule hiyo itatoa nafasi kwa vijana ambao wameshindwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano, kuwawezesha kujifunza stadi za ufundi zitakazowaandaa kupambana na changamoto za ajira.
“Shule hii itakuwa mkombozi wa vijana wetu. Hatuwezi kupuuza umuhimu wa mafunzo ya ufundi katika kupambana na ukosefu wa ajira. Nawataka wote mnaohusika kuhakikisha kazi hii inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyo bora,” amesema Mhe. Kasilda.
Mradi huu, unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 584 za Kitanzania kupitia mpango wa SEQUIP na unalenga kuleta mabadiliko ya kudumu katika maisha ya vijana. Mhe. Kasilda amehimiza umuhimu wa kutumia fedha hizo kwa uadilifu, akitaka kila shilingi itumike kufanikisha lengo lililokusudiwa.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Kasilda ameahidi kufuatilia maendeleo ya ujenzi mara kwa mara kuona shule hii inakamilika ifikapo Machi 15.
Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali ni zaidi ya mradi wa maendeleo ni mwangaza mpya kwa kizazi cha kesho, kuwapatia vijana ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuwawezesha kujenga maisha bora kwao na kwa jamii kwa ujumla.