Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Mkeyenge (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Bi. Isabela Maganga wakisaini mkataba wa makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya kifedha, mikataba hiyo imesainiwa leo Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Bi. Isabela Maganga akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini ya makubaliano ushirikiano wa suluhisho la Bima za kilimo na Mikopo ya Kidijiali na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini ya makubaliano ushirikiano wa suluhisho la Bima za kilimo na Mikopo ya Kidijiali na Benki ya Equity Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Mkeyenge Mkurugenzi , Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Isabela Maganga, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria NIC Asma Mohamed, Mkuu wa Kiengo cha Sheria Equity Benki Mugisha Mboneko wakionesha mikataba mara baada ya kuisaini jijini Dar es Salaam leo Januari 16, 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Kaimu Mkeyenge Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Isabela Maganga wakibadilishana mikataba.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Benki ya Equity Tanzania imeingia makubaliano ya Ushirikiano wa suluhisho la Bima za kilimo na Mikopo ya Kidijiali na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa ajili ya kufanya kazi pamoja jambo ambalo litasaidia benki hiyo kuwa na mtaji mzuri pamoja na kuwalinda wateja dhidi ya majanga mbalimbali katika biashara, mali, familia na kufikia malengo ya Serikali kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini ya makubaliano kati Benki ya Equity Tanzania na NIC, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania Bi. Isabela Maganga, amesema kwa kutambua uwezo na mkubwa wa NIC, benki ya Equity wameona ni vizuri kuwa na ushirikiano wa kimkakati ambao utawezesha taasisi hiyo kufanya kazi kwa ufanisi.
Maganga amesema kuwa katika ushirikiano huo wa kimkakati wamezingatia uhitaji mkubwa wa wateja wao pamoja na soko.
“Benki tumetoa kipaombele sekta ya kilimo na madaraja ya wateja hasa wafanyabiashara wadogo na wakati ambapo tunawafikia kwa njia ya kidijitali kwa kuwakopesha mitaji” amesema Maganga.
Amesema kuwa licha ya kuwawesha wateja kwa kuwakopesha mitaji, sasa wakati umefika wa kulindwa na majanga kupitia NIC ambao ni wadau muhimu katika kufikia malengo.
Maganga amesema kuwa huduma ya utoaji wa mikopo kwa njia ya kidijitali wameanza muda mrefu na mpaka kufika mwaka 2024 asilimia 67 ya wateja wamechukua mikopo kwa njia ya mtandao na kufanikiwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 300.
“Mwaka 2024 tumetoa mikopo kwa wateja 20,000 ambapo sasa wanapaswa kulindwa na majanga katika mitaji yao hasa biashara, mali pamoja na familia, hivyo tumeona tufanye kazi na NIC ili kufanikisha kuwalinda “ amesema Maganga.
Ameeleza kuwa benki ya Equity imekusudia kutoa huduma ya bima seka ya kilimo, huku akifafanua kuwa wanakopo katika benki hiyo watakuwa salama kwani wanakwenda kufanya kazi na NIC.
Amesisitiza kuwa wanaendelea kutoa elimu ya bima kwa wananchi ili kuhakikisha wanakuwa na uwelewa mkubwa katika kulinda mali zao na biashara kupitia bima.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge, amesema kuwa makubaliano hayo ya kibiashara yamelenga kusaidia uchumi wa Taifa kupiga hatua kupitia sekta ya fedha.
Mkeyenge amesema kuwa ni muhimu kuziwezesha benki za biashara kupata mitaji kupitia ada za bima wanazopata kwa wateja mbalimbali kama sehemu ya uwekezaji.
”Ukwasi ni muhimu kwa benki za biashara ili wananchi, kampuni zetu hapa nchini pamoja na wawekezaji mbalimbali waweze kukopesheka na kufanya shughuli za uchumi bila kuteteleka” amesema Bw. Mkeyenge.
Amesema kuwa makubaliano hayo yataiwezesha benki ya Equity kwa mtaji mzuri pamoja na kufanya uwekezaji wenye kuleta tija kwa Taifa.
“Mikopo itakuwa inakatiwa bima hasa seka ya kilimo, wanakopo katika benki Equity watakuwa salama”