*Aipongeza Bodi ya GST kwa utendaji uliotukuka
*Prof. Ikingura atoa tano kwa Menejiment ya GST
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameshiriki hafla fupi ya kuiaga Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambayo imefikia mwisho wa muda wake wa kuiongoza taasisi hiyo tangu kuteuliwa kwake mwaka 2022.
Waziri Mavunde ameishukuru Bodi hiyo kwa ushauri, miongozo na maelekezo yao yote waliyoyatoa kuhusu taasisi hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa yamesaidia kuibadisha GST katika muelekeo chanya.
Waziri Mavunde amebainisha hayo katika hafla ya kuwaaga Wajumbe hao iliyotanguliwa na kikao cha 21 cha Bodi ya GST ambayo imefikia mwisho wa kipindi chake cha kuisimamia taasisi hiyo baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Aidha, Waziri Mavunde amesema, malengo ya Serikali kupitia Wizara ya Madini ni kuona GST inajengewa uwezo ili iweze kufanya Majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa na kutimiza malengo ya taasisi kwa vitendo.
“GST ndiyo moyo wa Sekta ya Madini hivyo, ninatamani kuona GST inajengewa uwezo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo kuibua maeneo mapya yenye madini na hivyo kuvutia Uwekezaji mkubwa,” amesema Waziri Mavunde.
Kwa upande wake, Prof. Ikingura ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo kwa vipindi viwili tofauti. Aidha, amempongeza Waziri wa Madini, Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Menejimenti ya GST kwa ushirikiano waliompatia yeye na wajumbe wote wa Bodi hiyo na kuwasisitiza kuendelea kuwa na ushirikiano, upendo na umoja katika utumishi wao.
Naye, Katibu wa Bodi hiyo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amemshukuru Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi hiyo kwa miongozo, ushauri na maelekezo yote waliyoyatoa katika kipindi chote cha uongozi wao katika Taasisi hiyo.
Aidha, Dkt Budeba amesema, milango ya Menejimenti ya GST iko wazi kupokea ushauri, maoni na miongozo mbalimbali kutoka kwa Wajumbe hao na kuahidi kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo yote ya Bodi hiyo.
Wajumbe wa Bodi ya GST waliomaliza muda wao kuhudumu katika taasisi hiyo ni pamoja na Prof. Justinian Ikingura, Dkt. Dalaly Kafumu, Bertha Mwankusye, CPA. Constantine Mashoko, Dkt. AbdulRahman Mwanga, Mhandisi Yahya Samamba na Ramadhan Lwamo. Aidha, wajumbe wa Kamati za Bodi hiyo waliomaliza muda wao ni Augustine Olal, Mohamed Gombati, CPA. William Mtinya na Dkt. Kwelwa Shimba.