Na WAF Dar, es Salaam
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam inatarajia kuanza zoezi la umezeshaji wa Kingatiba dhidi ya magonjwa ya matende na mabusha au ngirimaji kwa wananchi waliopo kwenye kata 10 za wilaya hiyo zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa huo kuanzia Januari 22 hadi 26, 2025.
Hayo yamebainishwa leo Januari 15,2025 kwenye kikao cha Kamati ya Afya ngazi ya msingi kilicholenga kuweka mikakati ya kuanza kwa zoezi la umezeshaji wa kingatiba hizo kwa wananchi kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule.
Kata ambazo zinatarajiwa kufikiwa na zoezi hili ni pamoja na Kijitonyama, Makumbusho, Kigogo, Ndugumbi, Hananasifu, Mzimuni, Tandale, Kinondoni, Magomeni na Mwananyamala ambapo zoezi hili limelenga kuwafikia watu zaidi ya 284,035.
“Wapo watu ambao tunaishi nao kwenye maeneo yetu bado wanasumbuliwa na mabusha na matende, huu ni ugonjwa mbaya na unaathiri shughuli za kijamii na uchumi wa familia zetu,” amesema Mhe. Mtambule.
Mhe. Mtambule amepongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa sekta kwa kuendelea kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za tiba na kinga nchini ikiwemo kutoa kingatiba hizo za ugonjwa wa matende na mabusha katika wilaya ya Kinondoni.
Katika hatua nyingine Mhe. Mtambule ameitaka Kamati ya Afya ngazi ya Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kumeza kingatiba hizo ili waweze kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha huku akitoa onyo kali kwa wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya kuhujumu zoezi hilo kwa kwa kuwahadaa wananchi na taarifa za uongo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Peter Nsanya amesema kuwa Halmshauri inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na makundi maalum juu ya umuhimu wa kingatiba hizo.
Amebainisha kuwa zaidi ya wahudumu wa afya 146 wanaendelea na kazi ya kutoa elimu kwa wananchi.
Walengwa watakaomeza kingatiba hizo ni watu wote wenye umri kuanzia miaka mitano (5) na kuendelea huku huduma zitatolewa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, wagawa na walimu waliopewa mafunzo ya jinsi ya kugawa dawa hizo.
Zoezi la ugawaji wa Kingatiba hizo litafanyika kwa kupitia nyumba kwa nyumba kwenye makazi yetu, shuleni,ofisi za umma na binafsi,vituo vya kutolea huduma za afya,vituo vya usafiri, sokoni na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu.