*Kamati yaridhishwa na Kasi ya ukuaji wa Taasisi hiyo.
Na Beatus Maganja, Dodoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis R. Semfuko akiambatana na Menejimenti ya TAWA leo Januari 10, 2025 amewasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TAWA kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Augustine Vuma Holle (Mb) katika kikao kilichofanyika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Akiwasilisha taarifa hiyo Semfuko amesema TAWA imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inaongeza mapato Serikalini huku akibainisha uwindaji wa kitalii kuwa chanzo kikuu cha mapato ya TAWA ambapo huchangia takribani 70% ya mapato.
Semfuko amesema baada ya UVIKO 19 mapato ya TAWA yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka Shillingi Billioni 25.75 mwaka 2020/21 hadi shillingi bilioni 55.57 mwaka 2022/23 na kuongeza kuwa mapato hayo yalizidi kuongezeka kufikia bilioni 75.96 mwaka 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 37 ukilinganisha na mwaka 2022/23 kutokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Mamlaka ikiwemo uwekezaji mahiri (SWICA), kuboresha miundombinu, kutangaza fursa za uwekezaji na kuendelea kugawa Vitalu vya uwindaji wa kitalii Kwa njia ya mnada wa Kielekroniki.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Bodi ya TAWA amesema TAWA imeandaa Mkakati mahsusi wa kuongeza mapato wa miaka minne 2024/25 – 2027/28 ambao unalenga kuongeza mapato kufikia Shillingi Billioni 189 ifikapo mwaka 2027/28 jambo ambalo amesisitiza kuwa litaiwezesha Taasisi hiyo kuchangia katika mfuko wa Mkuu wa Serikali kiasi zaidi ya inachopokea.
Vilevile Semfuko amesema TAWA imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inahusisha kuboresha miundombinu ya utalii, ununuzi wa vitendea kazi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, miradi inayotajwa kuleta mafanikio makubwa katika nyanja za utalii na uhifadhi.
Akitaja mafanikio yanayotokana na uwekezaji huo Semfuko amesema watalii wa picha waliongezeka kutoka 37, 684 mwaka 2020/21 hadi watalii 194,180 mwaka 2023/24 ambao inajumuisha watalii 1,047 kutoka katika meli 9 za kitalii waliotembelea Hifadhi ya urithi wa dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati ya PIC wameipongeza TAWA Kwa hatua za ukuaji wa kasi kimapato pamoja na uwajibikaji katika mapambano dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu.
“Kwakweli TAWA wameonesha “Progress” kubwa sana kwenye utendaji wa kazi, mapato na hata mabadiliko ya Shirika lenyewe pia tumeona kuna hatua kubwa sana ya ukuaji” amesema Mhe. Dkt. Pius Chaya Mbunge wa Manyoni Mashariki.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mhe. Augustine Vuma Holle licha ya kutoa pongezi kwa utendaji mzuri wa TAWA ameiagiza Taasisi hiyo kuendelea kuimarisha mikakati ya kukusanya mapato, kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuongeza matumizi ya teknolojia katika udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.