DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
Neema Ngowi, mjasiriamali wa Kijiji cha Makumbusho, amepongeza juhudi za kuandaa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28, 2025, jijini Dar es Salaam. Akizungumza na Fullshangweblog, Neema alisema mkutano huo ni fursa muhimu kwa wajasiriamali wa Tanzania, hasa wale wanaojihusisha na uuzaji wa bidhaa za mikono wakati wa mikutano ya kimataifa.
Kwa niaba ya wajasiriamali wenzake, alionyesha furaha kwa ujio wa wageni kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya kushiriki mkutano huo, huku akieleza changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa taarifa za mapema kuhusu ushiriki wao.
Alisema mara nyingi wajasiriamali hukosa taarifa muhimu zinazowawezesha kujiandaa kikamilifu. “Tunaomba serikali itusaidie kwa kutupatia taarifa mapema pamoja na mwongozo wa moja kwa moja wa namna tunavyoweza kushiriki na kuuza bidhaa zetu,” alisema.
Neema alieleza kuwa mikutano ya kimataifa inaleta fursa kubwa kwa wajasiriamali wa ndani kutokana na mahitaji ya wageni wa bidhaa za asili za Tanzania kama batiki, viungo, asali, na dawa za miti shamba. “Kupitia biashara hizi, tunapata kipato, kuboresha maisha yetu, na kuchangia uchumi wa taifa,” alisisitiza.
Aidha, alibainisha kuwa wageni wanaokuja nchini huongeza mzunguko wa fedha za kigeni ambazo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania. “Fedha hizi zinapozunguka kwenye soko letu, zinainua uchumi wetu,” aliongeza.
Neema aliomba serikali kuhakikisha wajasiriamali wanapewa taarifa mapema kuhusu mikutano mikubwa kama huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, akisema kuwa maandalizi bora yatawawezesha kuwakilisha nchi kwa ubora zaidi.
Alitoa wito kwa wajasiriamali kuwa waaminifu na kujenga uzalendo kupitia bidhaa na huduma wanazotoa. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwa na uelewa wa msingi kuhusu nchi ili kujibu maswali ya wageni kwa usahihi.
Kwa kumalizia, alitoa wito kwa waandaaji wa mikutano kuhakikisha wajasiriamali wa ndani wanashirikishwa ili waweze kunufaika zaidi na fursa za kiuchumi zinazotokana na mikutano ya kimataifa.