Timu ya mchezo wa Jokgu ya Space imefanikiwa kutwaa ubingwa katika bonanza maalum la kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, lililofanyika kwenye viwanja vya Mnazimmoja, mjini Unguja.
Space, ikiongozwa na mkufunzi wao Master Kim, ilionyesha umahiri mkubwa na kufanikiwa kuibwaga timu ya Mbweni A kwa jumla ya seti 2-0 katika fainali yenye ushindani wa hali ya juu.
Mgeni rasmi wa tukio hilo alikuwa Balozi wa Vijana Zanzibar, Mohammed Kassim Mohammed, maarufu kama Prince Eddycool. Alishuhudia mchezo uliojaa mbinu, ari, na ushindani kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Space ilianza kuonyesha dalili za ushindi mapema kwa uchezaji uliotawaliwa na mbinu bora, huku Mbweni A wakionyesha nia ya kushinda kwa kila hali. Katika seti ya kwanza, Mbweni A walionekana kuwa na nafasi kubwa ya ushindi, lakini Space walipambana na kuibuka na ushindi wa seti hiyo kwa alama 15-13.
Seti ya pili ilishuhudia mapambano makali, ambapo Mbweni A walionyesha ustadi mkubwa mwanzoni, lakini walipoteza mwelekeo dakika za mwisho. Space walitumia makosa ya wapinzani wao na kumaliza seti hiyo kwa alama 15-14, hivyo kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Mashindano hayo yalihusisha timu nne:
1. Space – Nafasi ya kwanza.
2. Mbweni A – Nafasi ya pili.
3. Mbweni B – Nafasi ya tatu.
4. Shakani – Nafasi ya nne.
Balozi wa Vijana, Prince Eddycool, alisifu juhudi za timu zote na kueleza kuwa mashindano hayo yameonyesha vipaji vya hali ya juu miongoni mwa vijana wa Zanzibar. Alitoa wito kwa vijana kuendelea kushiriki michezo kama njia ya kukuza vipaji na kujenga mahusiano ya kimataifa kupitia michezo ya utamaduni kama Jokgu.
Mashindano ya Jokgu yameacha alama muhimu kwa vijana wa Zanzibar, si tu katika kusherehekea Mapinduzi, bali pia katika kujifunza michezo mipya na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Timu ya Space sasa inajivunia kuwa mabingwa wa kwanza wa mchezo huo visiwani Zanzibar, hatua inayotarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya michezo ya aina hiyo katika siku zijazo.