Balozi wa Vijana Zanzibar, Mohammed Kassim Mohammed, maarufu kama Prince Eddycool, amepongeza hatua ya raia wa Korea Kusini kuleta michezo ya tamaduni zao visiwani Zanzibar, akisema kuwa ni ishara ya utayari wao kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya michezo.
Prince Eddycool alitoa kauli hiyo wakati akifungua mashindano ya Kombe la Mapinduzi kupitia michezo ya Kikorea, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazimmoja, Wilaya ya Mjini Unguja.
Alieleza kuwa hatua ya vijana wa Zanzibar kujifunza michezo hiyo si tu inawapatia fursa ya kuelewa tamaduni za Korea Kusini, bali pia inachangia kukuza na kuibua vipaji vipya vitakavyotangaza Zanzibar kimataifa.
“Vijana wa Zanzibar wanapaswa kutumia fursa hii kujifunza kwa bidii. Mchezo huu unaweza kuwapatia fursa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujenga urafiki wa kudumu na Korea Kusini. Nimefurahishwa kuona jinsi vijana walivyojitahidi, na sasa ni jukumu letu kuwashajiisha vijana wengi zaidi kujiunga na michezo hii,” alisema.
Aidha, Prince Eddycool alihimiza vijana kuwa na nidhamu, kujipanga, na kufuata maelekezo ya mchezo huo ili kunufaika nao. Pia aliwashauri viongozi wa Taasisi ya Utamaduni wa Korea Zanzibar (KCFZ) kuhakikisha wanatoa vifaa stahiki kwa wachezaji ili kuhakikisha usalama wao wanaposhiriki michezo hiyo.
Mkufunzi wa michezo hiyo, Master Kim Jengueh, alifafanua kuwa mashindano hayo yalilenga kuitangaza michezo ya utamaduni wa Korea Kusini, huku pia wakiungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi.
Katika mashindano hayo, timu nne zilishiriki: Shakani, Mbweni A, Mbweni B, na Space. Timu ya Space ilitwaa ubingwa kwa kuwashinda Mbweni A kwa seti 2-0.
Mrajisi wa Vyama vya Michezo Zanzibar, Abuubakar Mohammed Nunda, alibainisha kuwa mchezo huo, ambao asili yake ni Korea Kusini, unafanana sana na volleyball, jambo linalowafanya vijana wa Zanzibar kuwa na uwezo mkubwa wa kuucheza.
“Tumeshakamilisha usajili wa mchezo huu ili kuwa sehemu ya michezo inayotambuliwa, na tunaamini utaongeza nafasi ya Zanzibar kupata wanachama katika vilabu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi. Lengo letu ni kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha michezo,” alisema Nunda.
Aidha, alibainisha kuwa Zanzibar pia ina mpango wa kueneza michezo yake ya kitamaduni kwa nchi jirani. Kwa sasa, tayari urafiki kupitia michezo umeanzishwa na Malawi, hatua itakayochangia kuimarisha mahusiano ya kijamii na kiutamaduni.
Hatua ya Wakorea kuleta michezo ya tamaduni zao Zanzibar inatoa fursa ya kipekee kwa vijana wa Zanzibar kujifunza, kushirikiana, na kujitangaza kimataifa kupitia michezo. Viongozi wa Serikali na wadau wa michezo wanatarajiwa kuendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha michezo inakuwa chachu ya maendeleo ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni wa visiwani humo.