Na Prisca Libaga, Arusha
Serikali kupitia wizara ya afya imepongeza Hospitali ya rufaa ya Mout Meru kwa kuanzisha miradi ya kibunifu ambayo inawezesha wananchi kupata huduma bora za afya.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Mh. Jenista Mhagama wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya Mount Meru katika ziara yake ya kukagua huduma za afya pamoja na kuzindua huduma za dharura kwa watu maalum katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru.
“Nimefurahishwa na ubunifu mkubwa wa utoaji huduma za afya kupitia mifumo ya mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mgonjwa na daktari hapa hospitali ya mount meru jambo ambalo linaongeza uwajibikaji kwa watumishi na hospitali zingine zinapaswa kujifunza hapa Mount Meru hospitali”amesema Waziri Jenista Mhagama
Aidha Mh.Mhagama Amesema kuwa kutokana na huduma bora zinazotolewa Mount Meru Hospitali, serikali ipo tayari kuwekeza kwa kujenga jengo kubwa jipya la kisasa la magonjwa ya nje yaani(OPD) ili kuendelea kuimirisha huduma bora za afya kwa kuzingatia kuwa Mkoa wa Arusha ni kituo kikubwa cha utalii na mikutano ya kimataifa.
Waziri Jenista Mhagama katika ziara yake Mount Meru Hospitali amezindua rasmi huduma ya dharura kwa watu maalumu ambapo itatoa huduma kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa, wakuu wa mashirika,watalii pamoja na wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh Paul Makonda ampongeza hospitali ya Mount Meru kwa huduma bora za afya zinazotolewa na kusema kuwa kwamba hana mashaka na Utoaji wa huduma za afya za hospitali ya mount meru.
Naye Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount meru Dkt. Alex Ernest ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongezewa watumishi wa kada ya afya wapatao 71 ili kuedelea kuwezesha ufanisi wa huduma bora za afya .
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru imeendelea kuwa kinara katika utoaji huduma bora za afya,ubunifu katika sekta ya afya na hivyo kuendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.