Na Ashrack Miraji, Fullshangwe Media
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, Mwalimu Neema Limunge, amesema kuwa mabadiliko ya mtaala mpya yanakuja na umuhimu wa kuwajengea uwezo wakuu wa shule na walimu ili waweze kuelewa na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha walimu na wakuu wa shule, Mwalimu Limunge alisema ni muhimu kwa walimu kuelewa vigezo vya mtahani mpya na kujiandaa vyema kabla ya kuanza kufundisha.
“Mbali na kuwajengea uwezo kuhusu mtaala mpya, tumefanya tathmini ya matokeo ya kidato cha pili. Tumejipima, tukaona tulipo na tunatakiwa kufika wapi. Kwa hiyo, tumekubaliana mikakati ya kuboresha utendaji na kuondoa matokeo duni kama division zero na division four,” alisema Mwalimu Neema Limunge.
Aliongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kuwa wilaya hiyo inakuwa na matokeo bora zaidi, huku wakitarajia kuwa na division one na two pekee. “Tunatamani sana kuwa na division one na mbili pekee. Tunapozungumza kuhusu elimu, tunasisitiza misingi ya kujifunza na ufundishaji bora kwa watoto wetu waliopo mashuleni,” alisema Mwalimu Limunge.
Mwalimu Neema Limunge pia alisisitiza kuwa mwaka 2025 utakuwa ni mwaka wa mabadiliko makubwa, kwani walimu wameonyesha hamasa ya kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora. “Mwaka huu 2025 utakuwa ni mwaka wa mfano kwa sababu tumedhamiria kufanya kazi kwa juhudi na kuleta mabadiliko katika shule zetu hapa Same,” alisema.
Afisa Elimu huyo aliishukuru serikali ya awamu ya sita kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu. Alisema Serikali imejizatiti katika kujenga miundombinu ya shule ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora. “Nashukuru sana kwa kazi kubwa inayofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu, hasa katika kujenga shule mpya na kuweka mazingira bora kwa watoto wetu,” alisema Mwalimu Limunge.
Aidha, Mwalimu Josephine alielezea umuhimu wa kuboresha mazingira ya shule ili kuzuia matatizo kama mimba za utotoni na ukatishaji wa masomo. Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa walimu na jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira salama na bora. “Lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanajifunza katika mazingira salama, bila kuathiriwa na matatizo kama mimba za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za utotoni,” alisema Mwalimu Josephine.
Sambamba na hayo, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na mitaala iliyoboreshwa, ambayo ni sehemu ya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini. Uzinduzi wa sera hiyo utafanyika Januari 31, 2025, katika ukumbi wa CCM Jakaya Kikwete, Dodoma.