MKURUNGENZI Mtendaji Hospitali ya Shree Hindu Mandal, Dar es Salaam,dk Kaushik Laxmidas Ramaiya ametunukiwa tuzo ya heshima ya juu zaidi kutokana huduma ya kipekee kwa jamii katika uwanja wa dawa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa India nchini, imesema tuzo hiyo imetolewa mnamo terehe 10Januari,2025 na Rais wa India kwenye Kongamano la 18 la tuzo hizo lililofanyika Bhubaneswar.
Dk Ramaiya ambaye pia ni Mshauri katika hospitali hiyo ni raia wa Tanzania mwenye asili ya India, amejitolea kwa miaka mingi kufanya utafiti kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na mengine pia amekuwa akishauri wagonjwa kuwa uvumilivu hasa wawapo kwenye hatari za magonjwa ya moyo na mishipa.
“Pamoja na kutoa ushauri anafanya kazi na kutibu kikamilifu watoto walio na kisukari cha aina ya 1, kisukari cha ujauzito, ugonjwa wa kimetaboliki na matatizo ya moyo na mishipa ya dawa za kupunguza makali ya VVU/UKIMWI pamoja na TB,”ilieleza taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo imesema kabla ya kutolewa tuzo hizo kuliandaliwa Kongamano lililoongozwa na vikao vyenye mada mbalimbali ilikusirikisha wageni mashuhuri kutoka Mataifa mengine wakiwemo wajasiliamali, wafanyabiashara na wengine wengi.
Serikali ya India imekuwa ikitekeleza mpango huo wa Utoaji tuzo mahususi ya diaspora lengo ikiwa ni kukuza uhusiano wake na nchi mbalimbali jumuiya yake ya kimataifa ya Wahindi. Juhudi hizi zimesaidia na kuleta mafanikio makubwa na kudumisha uhusiano mkubwa wa kihisia kati ya diaspora na India.