Watendaji wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Manyara wametakiwa kuendelea kulipa madeni yao kwa Bohari ya Dawa (MSD), ili kuiwezesha taasisi hiyo kuwa na mtaji wa kutosha kwa ununuzi wa bidhaa za afya zinazotolewa kwenye vituo vya afya kote nchini.
Hayo yalisemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Method, wakati akifungua kikao cha wadau na wateja wa MSD kanda ya Kilimanjaro, kilichoshirikisha wawakilishi wa mkoa huo.
Dkt. Method alisisitiza kuwa malipo ya madeni kwa MSD yanachangia kwa kiasi kikubwa ubora wa huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya, na hivyo ni muhimu kwa watendaji kuimarisha ushirikiano wao na MSD.
“Pamoja na kulipa madeni yetu kwa MSD, ni muhimu kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na taasisi yetu hii. Tukikumbana na changamoto, tuketi pamoja kuzitatua ili kuondoa malalamiko ya wananchi, ambao ndio wapokea huduma,” alisema Dkt. Method.
Aidha, Dkt. Method aliipongeza MSD kwa kuboresha huduma zake katika Mkoa wa Manyara, ambapo upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka na kufikia asilimia 95. Alisema mafanikio haya ni hatua kubwa inayosaidia kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Dkt. Vicent Gyunda, aliyeshiriki kikao hicho, alisema kuwa vikao vya wadau vina umuhimu mkubwa kwa MSD na wateja wake.
“Vikao hivi vinaisaidia MSD kupata mrejesho kutoka kwetu, ambao ni wateja wao. Pia, vimechangia ongezeko la upatikanaji wa bidhaa za afya hadi asilimia 98 katika Wilaya ya Kiteto,” alisema Dkt. Gyunda.
Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kushirikiana kati ya MSD na vituo vya kutolea huduma za afya ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa bidhaa za afya na kuboresha huduma kwa wananchi.