Na Fauzia Mussa
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, amesisitiza umuhimu wa kuelimisha wananchi kuhusu maendeleo yaliyofanywa na viongozi wakuu wa nchi kupitia njia mbalimbali ili kuimarisha uelewa na kuthamini mafanikio hayo.
Kitwana aliyasema hayo wakati akizindua kitabu cha Keeping the Legacy of the Tanzania Leadership toleo la kwanza, kilichoandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali, DEVCOM. Uzinduzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Kikwajuni, Mjini Unguja.
Alisema kitabu hicho kimekusanya maendeleo na mafanikio yaliyofanywa na viongozi wa Serikali zote mbili kwa awamu mbalimbali, lengo likiwa ni kuyahifadhi na kuyarithisha kwa vizazi vijavyo.
> “Kuzinduliwa kwa kitabu hiki ni hatua muhimu ya kuyarithisha mazuri ya viongozi wetu kizazi hadi kizazi,” alisema Kitwana.
Aidha, Kitwana alibainisha kuwa kitabu hicho kinaeleza mambo mengi ambayo hayajulikani kwa wengi na akawataka wananchi kukisoma na kukisambaza ili taarifa za maendeleo ya Tanzania tangu uhuru zipate kufahamika zaidi.
Aliongeza kuwa mbali na kuwaelimisha wazawa, kitabu hicho pia ni kivutio kwa wageni kwa kuwa kinaonyesha hatua za maendeleo katika sekta mbalimbali kama maji, umeme, na uchumi wa buluu.
Kwa mujibu wa Kitwana, kitabu hicho kinaweza pia kutumika kama marejeo kwa wanafunzi wa fani za uchumi na siasa ili kujifunza namna Tanzania ilivyopiga hatua za maendeleo na inavyotarajia kuendelea katika siku zijazo.
DEVCOM YAWA NA MAONO YA KUDUMISHA URITHI WA VIONGOZI
Mkurugenzi Mtendaji wa DEVCOM, Gaston Modest Kaziri, alisema kuwa toleo hilo ni la kwanza kuchapishwa, na matoleo mengine yatafuata kila mwaka hadi 2030. Lengo kuu ni kuweka kumbukumbu ya mazuri yaliyofanywa na viongozi wa nchi na kuyahifadhi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kaziri alieleza kuwa kupitia vitabu hivyo, viongozi wa baadae watajifunza kutoka kwa mafanikio ya waliotangulia, huku akisisitiza azma ya taasisi yao ya kuwafikia Watanzania wote, ndani na nje ya nchi.
KITABU CHA HISTORIA NA MAENDELEO
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mhandisi Salha Mohammed Kassim, alisema kitabu hicho kinaelezea historia za viongozi waliowahi kushika hatamu za uongozi kuanzia awamu ya kwanza hadi awamu ya sasa.
Aliongeza kuwa kupitia kitabu hicho, wananchi watajifunza kuhusu maendeleo yaliyopatikana katika muda mfupi wa Serikali ya awamu ya sita na nane, na kwamba kitabu hicho kitaendelea kuwa sehemu ya kumbukumbu na marejeo kwa wale ambao hawakushuhudia maendeleo hayo.
Washiriki wa uzinduzi huo waliishauri DEVCOM kuweka bei rafiki kwa kipato cha wananchi wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kunufaika na yaliyomo. Aidha, walipendekeza matoleo yajayo yatenganishe lugha za Kiswahili na Kiingereza ili kuwezesha uelewa mpana ndani na nje ya Tanzania.