Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto Wilaya ya Chato, Hezron Yuda,akizungumza na wajawazito ktika hospitali ya wilaya hiyo, leo kabla ya kuwakabidhi vifaa vya kujifungulia.
Mmoja wa wajawazito akipokea vifaa vya kujifungulia kutoka kwa Mratibu wa Afya ya Uzazi Wilaya ya Chato, Hezron Yuda, leo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato,Thomas Dime (kulia),leo akimkabidhi mmoja wa wajawazito kifurushi cha msaada wa vifaa vya kujifungulia vilivyotolewa na kikundi cha NUDBA Group ya Canada .
Wajawazito 50 wanaopata huduma katika kituo cha Afya Buseresere wilayani Chato,leo wakiwa amebeba vifurushi vya vifaa vya kujifungulia, vilivyotolewa na kikundi cha NUDBA Group ya Canada.
Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto, Hezron Yuda, leo akimkabidhi mmoja wa wajawazito katika kituo cha Afya Buseresere, wilayani Chato,msaada wa vifaa vya kujifungulia vilivyotolewa na NUDBA Group kupitia The Desk & Chair Foundation.
Wajawazito 60 wanaohudumiwa katika kituo cha Afya Bwanga, Chato mkoani Geita,leo wakiwa wamebeba vifurushi vya msaada wa vifaa vya kujifungulia, vilivyotolewa na Kundi la NUDBA Group kupitia The Desk & Chair Foundation.
Mmoja wa wajawazito wanaohudumiwa katika Kituo cha Afya Mapinduzi, wilayani Chato, leo akipokea msaada wa vifaa vya uzazi kutoka kwa Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto, wilayni humo, Hezron Yuda.
Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Mapinduzi, akiishukuru taasisi ya The Desk & Chair Foundation, leo baada ya kukabidhi vifaa vya uzazi vilivyotolewa na NUDBA Group kwa wajawazito 20.
Wajawazito wa kituo cha Afya Mapunduzi wakifurahi baada ya kupokea msaada wa vifaa vya kujifungulia, vilivyotolewa na Kundi la NUDBA la Canada na kukabidhiwa leo,na The Desk & Chair Foundation. (Picha zote na Baltazar Mashaka)
…………..
NA BALTAZAR MASHAKA,CHATO
AKINAMAMA wajawazito zaidi ya 140, wilayani Chato,katika Mkoa wa Geita,wamenufaika kwa vifaa vya uzazi vyenye thamani ya vilivyotolewa msaada na kikundi cha NUDBA cha Toronto,nchini Canada.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 7 vilivyokabidhiwa kwa walengwa na The Desk & Chair Foundation,ni ufadhili wa akinamama wa kikundi cha NUDBA Group, wakiadhimisha miaka 20 tangu kimeanzishwa.
Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation,Alhaji Dk.Sibtain Meghjee,amesema leo kuwa, msaada huo utawapunguzia akina mama wajawazito wenye hali duni kimaisha na wasio na uwezo kiuchumi, changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kujifungulia .
“Kutokana na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kujifungulia akinamama wajawazito wanapokwenda kujifungua katika vituo vya kutolea huduma za afya,wilaya iliomba vifaa hivyo katika taasisi yetu,hivyo tumewakabidhi viwasaidie akinamama,”amesema .
kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato (DAS),Thomas Dime,amesema msaada huo wa vifaa vya uzazi,vitawasaidia wajawazito zaidi ya 140 wanaotarajia kujifungua.
“The Desk & Chair Foundation,ni marafiki wa kweli na wamekuwa wakituletea msaada wa viti mwendo.Kwa niaba ya uongozi wa Wilaya ya Chato,niwapongeze na kuwashukuru,tufikishieni salamu kwa wafadhili na mkumbe Chato ni eneo lenu la kazi, endeleeni kutuunga mkono,”amesema.
Muuguzi wa Kituo cha Afya Bwanga,Enice Mwavika, amesema kituo hicho kwa mwezi kinahudumia wajawazito 550 hadi 600,lakini wengi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za kufanya maandalizi kabla ya kujifungua,sababu wanatoka familia duni kimaisha.
“Changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kujifungulia ni kubwa na uwezo unatofautiana,baadhi wanaweza kufanya maandalizi lakini mwengine hadi anakuja kujifungua hana maandalizi yoyote,”amesema.
Kwa sababu hiyo Mwavika amesema, baadhi yao hulazimika kutumia vifaa duni visivyo salama ambavyo vinahatarisha afya na usalama wao na kuishukuru The Desk & Chair Foundation kwa msaada huo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto Wilaya ya Chato,Hezron Yuda,kwa mwezi wanahudumia wajawazito kati ya 1800 hadi 2000, katika vituo 41 vya kutolea huduma.
“Tunashukuru msaada huu wa delivery park (vifaa vya kujifungulia), vitawasaidia akinamama wanapokwenda kujifungua,kuna uno bag,canura,catheter,urine bag (mfuko wa mkojo),maternity pad,macintosh na cotton hool(pamba) na vingine,hii inashiria kuwa mama wa uchumi wa chini wasio na uwezo wa kupata hivyo vifaa wamepata neema kwao,wanapokwenda kujifungua wasipate changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba,”amesema.
Yuda amesema vifaa hivyo vitaongeza chachu kwa wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea tiba pia, chachu ya kupata huduma bora za afya ya uzazi na kuomba wadau kuendelea kusaidia ili kukidhi mahitaji ya vituo 41 mbali na vinne vilivyonufaika.
“Vituo vilivyonufaika kwa msaada huo ni vya Bwanga 60, Mapinduzi 20,Buseresere 50a na Hospitali ya Wilaya 10.Tukipata msaada zaidi tutaongeza chachu na tunawashukuru,endeleeni kutusaidia ili kuwafikia wanawake wengi na tumefarijika kwa kugusa huduma ya afya ya mama na mtoto,”amesema.
Baadhi ya akinamama hao wajawazito wameomba juhudi zaidi zifanyike kwa wadau mbalimbali kusaidia vifaa hivyo kuepuka kutumia vifaa duni visivyo salama wakati wa kujifungua