Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imepata mafanikio makubwa katika juhudi zake za kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya kwa kukamata jahazi kubwa lenye uwezo wa kubeba tani nane za dawa hizo kwa wakati mmoja. Jahazi hilo, ambalo limekuwa likihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya kwa miaka 28, lilikamatwa likiwa na kilo 448.3 za methamphetamine na heroin.
Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, jahazi hilo lilikamatwa kupitia operesheni maalum iliyofanyika Bahari ya Hindi, ikihusisha vyombo vya ulinzi na usalama. Operesheni hiyo pia ilisababisha kukamatwa kwa raia nane wa Pakistani waliokuwa wakisafiri na jahazi hilo.
“Kukamatwa kwa jahazi hili ni hatua kubwa katika mapambano yetu dhidi ya dawa za kulevya. Limekuwa likitumika kwa muda mrefu kusafirisha dawa hizi, lakini juhudi za mamlaka zimezaa matunda,” alisema Lyimo wakati akizungumza leo jijini Dar es Salaam.
Kwa mwaka 2024 pekee, DCEA ilikamata kiasi cha kilogramu 2,327,983.66 za dawa za kulevya, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa nchini. Kati ya hizo, kilogramu 448.3 zilikamatwa ndani ya jahazi hilo, huku kilogramu nyingine 224.9 zikikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam.
Elimu na Tiba kwa Waraibu
Mbali na ukamataji wa dawa za kulevya, DCEA imeongeza nguvu katika kuelimisha jamii kuhusu madhara ya dawa hizo. Mwaka 2024, zaidi ya watu milioni 28 walifikiwa kupitia vyombo vya habari, matamasha, semina, na mikusanyiko mingine.
Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, pia imepanua huduma za matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya. Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kuwa vituo viwili vipya vya matibabu (MAT Clinics) vimeanzishwa katika mikoa ya Pwani na Tanga, kufikisha jumla ya vituo 18 nchini, ambavyo vinahudumia waraibu zaidi ya 18,000.
“Mafanikio haya yanaonyesha uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kupambana na tatizo hili. Pia, tumeimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na wadau wa ndani na nje ya nchi,” alisema.
DCEA pia ilijikita katika kufanikisha nyumba za upataji nafuu (sober houses), ambazo zimeongezeka kutoka 56 hadi 62 mwaka 2024, huku waraibu zaidi ya 17,000 wakipata huduma za utengamao.
Hatua Kubwa Katika Mapambano
Kamishna Lyimo aliongeza kuwa, kwa mara ya kwanza, dawa mpya ya kulevya aina ya 3-4 Methylene-Dioxy-Pyrovalerone (MDPV) ilikamatwa nchini. Alisisitiza kuwa mafanikio haya yanaakisi juhudi za mamlaka kuzuia usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, hatua ambayo imeimarisha ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha mikakati ya kupambana na dawa za kulevya, kuanzia udhibiti wa usafirishaji hadi utoaji wa huduma bora kwa waraibu.
“DCEA itaendelea kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya madhara ya dawa za kulevya,” alihitimisha Lyimo.