DAR ES SALAAM
Wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji mkoani Dar es Salaam wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuandaa na kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati, “Africa Energy Summit”ambao unatarajiwa kutafanyika Januari 27 hadi 28, 2025, kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa JINCC jijini Dar es Salaam.
George Masanje, Mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji wa abiria ya Bakwaya Tours and Safari, amesema kuwa hatua hiyo ya Rais Samia ni ya kihistoria na imeonyesha dhamira yake ya kuendeleza uchumi wa nchi na wananchi wake kupitia utalii wa mikutano ya kimataifa.
“Nampongeza sana Rais Samia kwa juhudi zake, hususan kupitia filamu ya The Royal Tour, ambayo imefungua milango ya utalii nchini. Mikutano kama huu ni fursa kubwa kwa sekta yetu kuchangia pato la taifa na kuboresha maisha yetu binafsi,” amesema Masanje.
Aidha, Masanje aliongeza kuwa kampuni yake ina magari zaidi ya 150 na ina uwezo wa kuhudumia wageni wengi kwa wakati mmoja, alitoa wito kwa wadau wa sekta ya usafirishaji kushirikiana kwa karibu na serikali ili kutumia fursa zinazojitokeza kwa ajili ya kujenga uchumi wao binafsi na serikali kwa ujumla kupitia kodi mbalimbali.
Masanje ameongeza kuwa wadau wa utalii na usafirishaji wanafurahia maendeleo haya, huku akitoa wito kwa wengine kushirikiana na serikali na kuendelea kumwombea Rais maisha marefu kwa juhudi zake za kuimarisha uchumi wa nchi.
“Hii mikutano inavyokuja hapa inatuinua sisi wadau wa sekta mbalimbali. Tunamshukuru sana Rais Samia na tunamwombea maisha marefu ili aendelee kutuletea fursa zaidi,” alihitimisha Masanje
Naye Stephen Kisanda, Meneja Masoko wa Bakwaya Tours and Safari, amesema kuwa kampuni hiyo imejipanga kuhudumia wageni wa ndani na nje ya nchi kupitia huduma za magari ya kukodisha aina mbalimbali yakiwemo ya viongozi na ya kifahari.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa juhudi zake za kulete mikutano mikubwa kama huu wa nishati nchini. Hii si tu inainua uchumi wa nchi, bali pia inatoa nafasi kwa wadau kama sisi kupata biashara na kupanua shughuli zetu,” amesema Kisanda.
Kisanda pia alitaja mafanikio ya mikutano mingine iliyofanyika nchini, kama vile mkutano wa SADC na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, akisisitiza kuwa hatua hizi zimeleta mabadiliko makubwa kwa sekta ya usafirishaji na uchumi kwa ujumla.