Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ephraim Mafuru akizungumza na Fullshangweblog kuhusu fursa zitakazopatikana katika mkutano wa “Africa Energy Summit”.
DAR ES SALAAM
NA JOHN BUKUKU
Bodi ya Utalii Tanzania imejipanga kutumia fursa ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) kwa kutangaza mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo wanyamapori kwa wageni zaidi ya 2,000 wanaotarajiwa kushiriki katika mkutano huo.
Akizungumza na Full Shangwe Blog leo jijini Dar es Salaam kuhusu fursa zinazopatikana katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Africa Energy Summit) utakaofanyika January 27 – 28, 2025, kwenye Ukumbi wa JINCC, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania Ephraim Mafuru, amesema kuwa bodi ya utalii imejipanga kutangaza vyanzo vyote vya utalii vilivyopo nchini ili kuleta tija kwa Taifa.
Mafuru amesema kuwa Tanzania kuna vyanzo vingi vya utalii ikiwemo utalii wa fukwe ambao Mkoa wa Dar es Salaam, Mafia pamoja na Zanzibar.
“Pia kuna hifadhi za Taifa ambazo zipo kanda ya kusini na kaskazini ikiwemo Serengeti, Mikumi, Nyerere, Ngorongoro pamoja na Mlima Kilimanjaro” amesema Mafuru.
Amesema kuwa Tanzania inafanya vizuri katika sekta ya utalii kwani mwaka 2024 wamefanikiwa kushinda tuzo nyingi Barani Afrika ikiwemo tuzo nne zinaonesha namna Taifa lilivyokuwa kivutio kikubwa cha utalii Duniani.
Ameeleza kuwa tuzo ya tano waliofanikiwa kupata kwa mwaka 2024 ni kuwa na kivutio kikubwa cha utalii wa safari duniani.
Mafuru amesema kuwa kwa mwaka 2025 wana nafasi nzuri ya kutangaza vivutio vya utalii kwa wageni ili wanapopanga kuja Tanzania waweze kuongeza idadi ya siku za kukaa nchini kwa ajili ya kuangalia utalii.