Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi mara baada ya kufungua Skuli ya Sekondari Misufini iliyopo Bumbwini Zanzibar tarehe 08 Januari, 2025.
………………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kusimamia malengo ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar ya kujenga ustawi wa wananchi ikiwemo kwa kuboresha sekta ya elimu.
Taarifa iliyotolewa na Sharifa B. Nyanga Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu leo Januari 08, 2025 imesema, Rais Dkt. Samia akizungumzia dhana pana ya Mapinduzi, amesema “Mapinduzi ni maendeleo, hatua baada ya hatua. Yale Mapinduzi ya kuutafuta Uhuru tulimaliza, sasa hivi ni Mapinduzi ya kutafuta maendeleo, hatua baada ya hatua, na kulinda Uhuru wetu; ndio Mapinduzi yetu sasa hivi”.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati akizindua Skuli ya Sekondari Bumbwini Misufini, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
Aidha, kutokana na mchango mkubwa wa Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, Rais Dkt. Samia ameelekeza skuli hiyo ibebe jina la kiongozi huyo kwa heshima yake.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa skuli hiyo ni matokeo ya maono ya Viongozi wa Mapinduzi waliodhamiria fursa ya elimu itolewe kwa watu wote, jambo ambalo limeendelea kusimamiwa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa hatua kubwa imepigwa katika sekta ya elimu huku idadi ya skuli pamoja na wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi sekondari ikiongezeka ikiwa ni matunda na matokeo ya Mapinduzi.
Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa shabaha ya Serikali zote mbili ni kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wanafunzi wenye utaalamu na ujuzi, utakavyowawezesha kushindana katika soko la ajira na kulinufaisha Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia umuhimu wa masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA), amesema kuwa Serikali inatekeleza Mkakati wa Uchumi wa Kidigitali ili kuwaandaa Watanzania kunufaika na ajira zinazozalishwa kupitia uwekezaji unaofanywa
nchini ikiwemo kuziwezesha shule/skuli kuwa na mifumo ya TEHAMA.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa wazazi kuwapa watoto wao nafasi ya kupata fursa ya elimu, ikiwemo kuwapatia muda wa kupitia masomo yao, kwenda shule/skuli wakiwa katika hali inayotakiwa.