Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii TTB, Bw. Ephraim Mafuru kushoto na Mkurugenzi Mtendaji wa Turkish Airlines Bw. Abdulkadir Karaman wakibadilishana nyaraka za makubaliano mara baada ya kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati yao kutangaza utalii wa Tanzania Katikati ni Mkurugenzi wa Utalii wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Dr. Thereza Mugobi.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii TTB, Bw. Ephraim Mafuru kushoto na Mkurugenzi Mtendaji wa Turkish Airlines Bw. Abdulkadir Karaman wakionesha nyaraka za mikataba hiyo zenye makubaliano mara baada ya kutia saini na kuanzisha ushirikiano kati yao kutangaza utalii wa Tanzania,
…………………
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeanzisha ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines) kwa mkataba wa miaka mitatu, ukiwalenga kukuza utalii wa Tanzania katika masoko ya kimataifa. Ushirikiano huo unalenga kutumia mtandao wa shirika hilo unaojumuisha zaidi ya ndege 490 zinazohudumia miji 350 duniani kote, zikiwemo 61 barani Afrika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru, alisema mpango huo unalenga kuongeza idadi ya watalii na wawekezaji nchini. Alisema Turkish Airlines itaonyesha vivutio vya Tanzania kwenye ndege, tovuti, na ofisi zao, huku pia wakitoa punguzo la nauli kwa wasafiri wa utalii.
“Huu ni mwanzo wa mikakati yetu ya kushirikiana na mashirika ya ndege. Tunatarajia kuvutia watalii wengi zaidi na pia wawekezaji, sambamba na kukuza sekta ya utalii na uchumi wa taifa,” alisema Mafuru, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kufanikisha makubaliano hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Turkish Airlines, Abdulkadir Karaman, alielezea shukrani kwa juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuweka mazingira salama ya biashara. Alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kufanikisha lengo la kuifanya Tanzania kuwa kivutio kikuu cha utalii duniani.
“Kauli mbiu yetu ni ‘Panua Ulimwengu Wako,’ na tuna rekodi ya Guinness kwa kusafiri hadi nchi nyingi zaidi duniani. Hii inathibitisha uwezo wetu wa kuunganisha watalii kutoka kila kona ya dunia hadi Tanzania,” alisema Karaman.
Akitangaza hatua mpya, alisema shirika hilo litaongeza safari zake nchini Tanzania kuanzia Juni, ambapo safari za Kilimanjaro zitaongezeka kutoka nne hadi 14 kwa wiki, na Zanzibar kutoka tisa hadi 14 kwa wiki.
Alihimiza wadau kutumia fursa za programu kama Touristanbul na Stopover mjini Istanbul, zinazowapa wasafiri uzoefu wa kipekee wanapopitia Istanbul kuelekea Tanzania.
Hatua hii ni ishara ya kuimarika kwa sekta ya utalii nchini kupitia ushirikiano wa kimataifa, huku TTB ikiahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine ili kufanikisha lengo la kuitangaza Tanzania ulimwenguni.