Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa (DMC) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Noel Kaganda Balozi Noel Kaganda akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari na wandishi wa habari iliyofanyika chuo kikuu cha Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
…………….
Kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusambaza umeme vijijini na uhamasishaji wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia umechangia kwa kiasi kikubwa Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Nishati unaotarajiwa Januari 27 hadi 28, 2025, katika Ukumbi wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa (DMC) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Noel Kaganda Balozi Noel Kaganda akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari na wandishi wa habari iliyofanyika chuo kikuu cha Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alisema Tanzania haikuchaguliwa kwa bahati mbaya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, isipokuwa imekidhi vigezo ambavyo waandaji wamejiridhisha navyo.
Balozi Kaganda alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na Tanzania kuwa ni moja ya nchi chache za Afrika zenye mipango thabiti ya kuwa na nishati ya kutosha na uhakika, mpango wa kusambaza umeme nchi nzima ikiwa ni pamoja na vijiji na vitongoji.
Aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na mikakati yake kabambe ya usambazaji na upatikanaji wa nishati ambapo malengo ifikapo 2030 asilimia 75 ya Watanzania wawe wamefikiwa na umeme na asilimia 80 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034
Alitaja Sababu nyingine kuwa ni kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania, amani na usalama na uzoefu wa kutosha wa kuwa nwenyeji wa mikutano mikubwa ambayo imekuwa ikifanyika nchini.
Mkutano huo unaandaliwa kwa ushirikiano baina ya Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Tanzania unalenga kuwakutanisha wakuu wa nchi zote za Afrika na wadau wengine ili kujadili kwa pamoja njia za kuchagiza upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Naye Mhandisi Jones Olotu, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini Wakala wa Nishati Vijijini (REA), akiwasilisha mada kuhusu usambazaji wa umeme vijijini amesema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Nishati, iliyoanzishwa kwa Sheria ya Nishati Vijijini Na. 8 ya mwaka 2005. Taasisi hiyo ilianza kazi rasmi mwezi Oktoba 2007 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2003.
Dhumuni la kuanzishwa kwa REA ni kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa vijijini kwa njia endelevu, kuchangia ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za kijamii kama afya, elimu, maji na mawasiliano, kuhifadhi mazingira, na kuimarisha usawa wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Mhandisi Olotu, hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imeboreshwa kwa kiwango kikubwa tangu REA ilipoanza kutekeleza majukumu yake.
Tulipotoka (2007): Vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 506 pekee, sawa na asilimia 2 ya wananchi wa vijijini.
Tulipo (2024): Hadi Desemba 31, 2024, jumla ya vijiji 12,301 kati ya 12,318 sawa na asilimia 99.9 vimeunganishwa na umeme.
Tunapokwenda (2025): Vijiji 17 vilivyobaki vinatarajiwa kufikishiwa umeme ifikapo Januari 31, 2025. Kwa upande wa vitongoji, 33,657 kati ya 64,359 sawa na asilimia 52.3 vimeunganishwa na umeme. Vitongoji vilivyosalia 30,702 vipo katika mpango wa miaka mitano kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kwa mujibu wa taarifa za NBS za mwaka 2020, wananchi wa vijijini wanaofikiwa na umeme ni asilimia 69.6, huku wastani wa kitaifa ukiwa asilimia 78.4. Kwa mujibu wa Sensa ya 2022, Tanzania Bara ina jumla ya watu 59,851,347, ambapo takriban watu 46,923,456 wanapata huduma ya umeme.
Hadi sasa, wananchi wanaopata huduma ya umeme vijijini ni 27,326,688. Thathmini mpya ya NBS kuhusu hali ya umeme vijijini inatarajiwa kuchapishwa Machi 2025.
Mhandisi Olotu alieleza mafanikio makubwa ya REA, ambayo ni pamoja na Kufikisha umeme katika vijiji 12,301 kati ya 12,318 sawa na asilimia 99.9., Kufikisha umeme katika vitongoji 33,657 kati ya 64,359 sawa na asilimia 52.3.
Eongeza kuwa mafanikio mengine ni Kuandaa mpango wa kupeleka umeme katika vitongoji 20,000 kati ya 30,702 vilivyosalia, Kuboresha maisha ya wananchi vijijini kwa kuwawezesha kupata fursa za uwekezaji kupitia huduma za umeme na upunguza wimbi la vijana kuhama vijijini kwenda mijini kwa kutengeneza fursa vijijini.