Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam (RAS) Dkt Toba Nguvila akizungumza na waandishi wa habari kuhusu muendelezo wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika Wilaya ya Ubungo ambayo imefanyika leo Jan 7,2024
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam (RAS) Dkt Toba Nguvila akipewa taarifa ya mradi na maafisa wa Manispaa ya Ubungo katika ziara ambayo imefanyika leo Jan 7,2024
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam (RAS) Dkt Toba Nguvila akifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya Hospitali ya Wilaya ya Ubungo iliyopo Kimara Baruti katika ziara ambayo imefanyika leo Jan 7,2024.
Mkuu wa Idara ya Afya lishe na Ustawi wa Jamii Manispaa ya Ubungo Dkt Tulitweni Mwinuka akizungumza na waandishi wa habari akieleleza namna wanavyosimamia sekta ya afya katika Manispaa hiyo katika ziara ambayo imefanyika leo Jan 7,2024.
……………………..
NA MUSSA KHALID
Serikali ya Mkoa wa Dar es salaam imesema ipo kwenye mpango wa kununua Mashine ya CT Scan kuipeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo iliyopo Kimara Baruti ili kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinatolewa katika hospitali hiyo.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam (RAS) Dkt Toba Nguvila wakati akizungumza kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika Wilaya hiyo akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo pamoja na watumishi wa Manispaa hiyo
Dkt Nguvila amempongeza Rais Dkt Samia Suluh Hassan kwa kuwapeleka huduma karibu wakazi wa Ubungo ili waweze kunufaika na huduma za afya.
Aidha amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ubungo kuhakikisha wanajenga uzio katika Hospitali hiyo ili kuondoa muingiliano wa wananchi na wagonjwa waweze kupata huduma katika mazingira mazuri.
Aidha amesema licha ya huduma inatolewa kwa hadhi ya Wilaya ni vyema wakaendelea kuongeza majengo katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuboresha huduma za Afya.
‘Adhma ya Mhe Rais ni kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinatolewa hapa hivyo ni lazima sisi watendaji kujitahidi kuweka kipaumbele kikubwa kwenye sekta ya afya’amesema Dkt Nguvila
Awali akizungumza Mkuu wa Idara ya Afya lishe na Ustawi wa Jamii Manispaa ya Ubungo Dkt Tulitweni Mwinuka amesema kuwa amesema hospitali hiyo ilianza mwaka 2022 na imeendelea kukua kutokana na wagonjwa kuongezeka kutoka 1200 kwa mwezi mpaka zaidi ya 6000.
Dkt Tulitweni amesema Hospitali hiyo inatoa huduma kwa kiwango ikiwemo mpango mkakati wa kuongeza jengo hilo ili liweze kukidhi Hospitali ya Wilaya ya Ubungo.
Nao Baadhi ya wananchi waliofika katika Hospitali hiyo kupata huduma wameipongeza serikali kwa kuwafikishia huduma kwa ukaribu ambayo imewaondolea changamoto ya kwenda umbali mrefu kutafuta huduma.
Mapema katika ziara hiyo Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam (RAS) Dkt Toba Nguvila alitembelea kuona Jengo la Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,pia amefanya ukaguzi katika Ujenzi wa Kituo cha Uwekezaji EACL,Ukaguzi wa ujenzi wa Barabara ya zege mrina km 0.56 na kukahua ukarabati wa soko la ndizi Mabibo.